KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Patrick Sibomana raia wa Rwanda amefunguka kuwa wao wanaelewa ugumu wa wapinzani wao, Simba lakini wana uhakika mkubwa wa kuwachapa katika mechi ya keshokutwa Jumapili kwenye Ligi Kuu Bara.
Kiungo huyo mwenye mabao matano katika ligi hiyo msimu huu, amesema hilo kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mechi hiyo, Yanga wanaingia wakiwa nafasi ya tatu na pointi 47 wakati Simba wao wakiwa kileleni kwa pointi 68.
Sibomana aliyesajiliwa wakati wa dirisha kubwa mwanzoni mwa msimu huu, amesema kwamba kwa upande wao wanajua wazi kwamba Simba ni timu ngumu na wanafanya vizuri katika ligi lakini wao watafanya kitu kikubwa kwa kujitahidi kuwafunga.
“Tunaelewa kwamba hii ni mechi kubwa na Simba lakini tutaonyesha kitu kizuri katika mechi hii ambacho kitawafanya mashabiki wetu wawe na furaha.
“Tutajitahidi kwa kiwango kikubwa tushinde mechi hii na kama kocha akinipa nafasi ya kucheza basi nitafunga kwa sababu hayo ni majukumu yangu ambayo natakiwa kuyafanya,” alisema Mnyarwanda huyo.
Stori: Said Ally, Dar es Salaam

