RAIS Magufuli kwa mara ya pili leo Machi 8, 2020 ameishuhudia Simba ikifungwa bao 1-0 na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Rais Magufuli ni shabiki wa Simba aliingia uwanjani hapo saa 10:40 jioni ikiwa ni muda mchache baada ya Rais wa CAF, Ahmed Ahmed kuingia uwanjani hapo.
Rais Magufuli alikuwa amevaa jezi yake ambayo nusu ilikuwa na rangi ya Yanga na upande mwingine rangi nyekundu huku akiwa amevaa kofia yenye rangi ya bendera ya Tanzania.
Leo Rais Magufuli akiwa amekaa jukwaani na mgeni wake rais wa CAF, Ahmed ameshuhudia Simba ikipokea kipigo kingine cha bao 1-0 kutoka kwa watani zao wa jadi.
Mshambuliaji Bernard Morrison alifunga bao pekee la Yanga kwa mpira wa adhabu katika dakika 44 na kuhamsha shangwe kwa mashabiki uwanjani hapo.
Mara ya mwisho Rais Magufuli alipokuwa uwanjani hapo alishuhudia Simba ikipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar msimu wa 2017/18.

