WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, William Lukuvi, amemaliza rasmi ulaji uliokuwa unafanywa na baadhi ya maafisa ardhi wa jiji la Arusha.
Amesema hayo mkoani Arusha, jana Machi 8, 2020 wakati wa ziara yake ya kuanzisha rasmi ofisi za ardhi za mikoa na kuvunja ofisi za kanda ambazo zilikuwa zinahudumia zaidi ya mkoa mmoja, hali iliyokuwa inawasababishia wananchi usumbufu.
Akizungumza na viongozi wa mkoa huo wakati wa hafla hiyo, amesema kuanzia sasa ulaji uliokuwa unafanywa na baadhi ya maafisa ardhi wa jiji kwa kudai posho za kwenda kufuatilia hati mkoa wa Kilimanjaro ameumaliza rasmi.
Ameongeza kuwa huduma zote za utoaji hati, uandaaji wa michoro ya mipango miji, na huduma za Msajili wa Hati zitatolewa katika Jiji la Arusha na si makao makuu ya Kanda Moshi kama ilivyokuwa hapo awali.
