
KATIKA kuadhimisha Wiki ya Macho Duniani ambayo hufanyika kila wiki ya pili ya mwezi Machi, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo Mloganzila imefanya zoezi la upimaji wa bure wa presha (shinikizo) ya macho ambapo takwimu zimeonyesha katika watu 65 watu tisa wamebainika kuwa na presha.


Wote waliobainika kuwa na tatizo hilo walipatiwa matibabu ya bure huku wengi wakipangiwa kuendelea na dozi.
Akizungumza na wanahabari, Daktari Bingwa wa Macho, Catherine Makunja, aliwaomba wananchi kupima afya yao ya macho mara kwa mara ili kama kuna tatizo litakalobainika mapema iwe rahisi kulikabili.

Naye Daktari Bingwa mwingine, Judith Mwende, aliwasisitiza wananchi kufanya hivyo na kusisitiza kuwa presha ya macho inaweza kukusababisha upofu wa ghafla bila kutegemea.

Baadhi ya watu waliofika kupata huduma hiyo waliusifu uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuwawezesha kupata bure huduma hiyo ambayo gharama zake ni kubwa mno na watu wengi walikuwa wanashindwa kuzimudu na kuishia kuwa vipofu.

HABARI:NEEMA ADRIAN
PICHA: RICHARD BUKOS/GPL