FAMILIA moja ya huko Gatuikira, kaunti ya Kiambu, Knya, ililazimika kufanya maziko kwa mtoto wao bila mwili wake baada ya kushindwa kulipa kiasi cha milioni 17 za Kenya.
Mwili wa Brian Kimani (13) ambaye alifariki Februari, mwaka huu, unazuiliwa katika Hospitali ya watoto ya Getruding ukiwa unadaiwa Ksh milioni 17.
Taarifa zinaeleza kuwa mtoto huyo alikuwa akitibiwa katika hospitali hiyo kwa takribani miezi mitano na nusu kwa ugonjwa wa Leukemia.
Katika ibada ya maziko hayo, familia na marafiki wa Brian walikusanyika katika Kanisa la ACK St. Stephens huko Gatuikira, Kaunti ya Kiambu, ambako kulikuwa na picha kubwa ya mtoto huyo kwenye altare.
Hata hivyo, mkuu wa huduma za tiba wa hospitali hiyo, Dr Thomas Ngwiri, amekanusha taasisi yao kuhusika na tukio hilo akisema si sera yao kuzuia mwili wa marehemu kwa kudai malipo.
“Kwa mujibu taratibu za huduma zetu na amri ya mahakama kuhusiana na suala hili, hospitali ilikubaliana na wazazi wa marehemu kubeba deni hilo na kuiruhusu familia hiyo kuuchukua mwili huo kwa maziko,” alisema Dr Ngwiri jana (Jumatano) akiongeza kwamba makubaliano yalikuwa ni kuuchukua mwili huo leo (Alhamisi, Machi 12) na kwamba hospitali yake ilikuwa inasubiri makubaliano hayo kutekelezwa.
Familia hiyo imekuwa ikihangaika kwa matibabu ya mtoto wao tangu Aprili, 2018, ambapo imetumia karibu Sh. milioni 30 za Kenya kwa matibabu yake nchini India na Kenya.
