YANGA imemaliza sherehe ya kuvuna ushindi dhidi ya Simba, mara baada ya kuchapwa na KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Salim Aiyeeh ndiye aliibuka shujaa kwa upande wa KMC, akifunga bao la ushindi kwa timu yake katika dakika ya 62 na kufufua matumaini kwa timu yake ya kusalia ligi kuu kwa msimu ujao, ambapo kwa ushindi huo wamefikisha pointi 30.
Yanga walianza mchezo huo kwa spidi ya juu ambapo dakika ya kwanza ya mchezo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alikosa bao baada ya shuti hafifu ambalo halikuwa na madhara katika mikono ya kipa wa KMC, Jonathan Nahimana.
KMC walijibu mapigo katika dakika ya pili kupitia kwa Kelvin Kijiri, aliyepiga shuti na kutoka nje ya lango, hivyohivyo kwa Hassan Kabunda aliyepiga shuti lililodakwa na kipa wa Yanga, Metacha Mnata.
Kwa jumla mchezo ulikuwa na spidi ndogo, huku timu zote zikijaribu kucheza kimbinu zaidi, ambapo dakika ya 29 Yanga waliamka na kutengeneza nafasi
kadhaa na kushuhudiwa Papy Tshishimbi akikosa bao, kupitia kwa Balama Mapinduzi dakika ya 38 na 42, ambaye alishindwa kufunga bao kwa kukosa utulivu.
Mpaka mapumziko ubao ulisoma Yanga 0-0 KMC, kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko kwa sababu timu zote zilishindwa kutengeneza nafasi nyingi, ambapo ilisubiriwa hadi dakika ya 50, ndipo Yanga wakatengeneza nafasi ya bao iliyoshindwa kutumiwa vema na Ditram Nchimbi.
KMC walitengeneza nafasi mbili tu, moja ikizaa bao, huku Yanga wakitengeneza nafasi tatu ambazo hazikuwa na hatari zozote. Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema: “Haukuwa mchezo mzuri kwetu kama unavyojua tumetoka kucheza mechi ngumu sana, baadhi ya wachezaji walikuwa na majeraha pia.
“Waliokuwepo walijitahidi kutengeneza nafasi ila walishindwa kuzitumia vizuri hivyo mchezo huu umepita tunaangalia mchezo wetu unaofuata dhidi ya Namungo,” alisema Luc.
Kwa matokeo hayo Yanga wanabaki katika nafasi ya tatu na pointi zao 50, wakiwa wamecheza michezo 26, ambapo keshokutwa Jumapili watakuwa na mchezo mwingine dhidi ya Namungo, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.



