MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema kutokana na ukimya kwa upande wa serikali kuhusu ombi lao la kuwepo maridhiano ya kitaifa walilolitoa kwa maandishi, chama hicho kimeamua kufanya mikutano nchi nzima kuanzia Aprili 4, mwaka huu bila kusubiri kibali cha mtu yeyote.
Mbowe amesema hayo leo Jumatatu, Machi 16, 2020, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu hali ya kisiasa nchini kulekea uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka huu, akisisitiza kuwa mikutano hiyo ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi huo.
“Nawatangazia viongozi wote wa Chadema, kanda, mikoa, wilaya, kata vijiji na misingi. Tuanze kufanya mikutano ya hadhara kwa utaratibu ulioko kisheria, kudai vitu viwili: Tume huru ya uchaguzi na demokrasia. Tupo tayari kwa lolote, hatumwogopi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wala asitutishe,” alisema Mbowe.
Tamko hilo ni miongoni mwa masuala kadhaa aliyoyazungumza siku chache tu baada ya kutoka gerezani ambako aliepuka kuendelea na kifungo kutokana na kulipa faini ambayo ilikuwa ni mbadala wa hukumu ya kifungo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Subira yetu, uvumilivu wetu na upole wetu umedharauliwa vya kutosha. Kama watatumia polisi na magereza kutufunga wote, watufunge. Tuko tayari kwa lolote. Kama wanafikiri mabomu, risasi na jela ni suluhu, basi wakatumie,” alisema.
Pia aliwapa pole baadhi ya makada wa chama hicho waliokumbana na tafrani ya vyombo vya usalama wakati walipokwenda kumpokea wakati wa kuachiliwa katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.
“Nawapa pole viongozi wote walioteswa siku ya Ijumaa walipokuja kunipokea, wako wengine wameumizwa lakini nawatia moyo. Safari yetu inakaribia asubuhi. Kwa hiyo nawapa pole Mdee, Kishoa, Bulaya na wengine wote waliofikwa na maradhi mbalimbali,” alisema huku akiongeza kwamba vyombo vya usalama vinaendesha kazi zao kwa kufuata maelekezo ya watawala na kuvibana vyama vya upinzani.