×

Achomwa Moto Akituhumiwa Kuiba Mahindi Shambani

POLISI mkoani Shinyanga linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwanamme anayekadiriwa kuwa na umri wa 25-30 ambaye hajafahamika jina wala makazi, aliyepigwa na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira  Mtaa wa Mwime wilayani Kahama akituhumiwa kuiba mahindi shambani.

 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba,  ilisema  tukio hilo limetokea Machi 15 mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri ambapo wananchi wa mtaa huo walimkamata marehemu akiiba mahindi katika shamba la mmoja wa wakazi wa mtaa huo.

 

Alisema kuwa baada ya kumkamata wananchi hao walijichukulia hatua mkononi kwa kumpiga na kisha kumchoma moto na kufariki dunia papohapo na kisha wao kutokomea kusikojulikana.

 

“Katika eneo la tukio kulikuwa na mahindi na baiskeli karibu na mwili wa marehemu kiashiria kwamba alitumia usafiri huo kubeba mahindi,” alisema.

 

Alifafanua kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama na chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali (mahindi) na jitihada za kuwatafuta waliohusika na mauaji hayo zinaendelea ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

NA; SALVATORY NTANDU

Leave a Comment