×

Wawa: Yanga Wasahau Kwenda Caf

BEKI wa kati wa Simba, Muivory Coast, Pascal Wawa, amefunguka kuwa kwa sasa wapinzani wao wakiwemo Yanga wanatakiwa kusahau juu ya kushiriki katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwani hawataweza kuufikia ubingwa wa msimu huu.

 

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 71 huku ikibakiza mechi 10 kumaliza Ligi Kuu Bara, tofauti na Yanga iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 wakati imebakiza mechi 11 kabla ya kumaliza ligi.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Wawa alisema kuwa mbali ya Yanga, hakuna timu yoyote itakayoweza kufikia pointi zao kwa sasa huku akisisitiza wanataka kushinda mechi zao zote zilizobakia.

“Kitu kikubwa ni kuhakikisha tunachukua ubingwa ambao naona umeshakaa kwenye njia yetu zaidi ni kuendeleza mapambano katika sehemu iliyobakia ili kufikia malengo yetu kwa sababu tuna alama nyingi zaidi.

 

“Nadhani jambo kubwa kwetu ni ubingwa na hakuna wa kuweza kutufikia kwa sasa maana tunachokiangalia ni michuano ya kimataifa, wapinzani wetu hakuna wa kufikia tulipo maana tunataka kushinda kila mchezo, hivyo inatusaidia kufikia malengo ya ubingwa, wao sina uhakika kama wataweza,” alisema Wawa.

Leave a Comment