SHAHIDI wa tatu katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, Sengwe Mbaruku, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima mkoani Kigoma (Mviwata) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kiongozi huyo anashtakiwa kwa kosa la kuwasemea wananchi wa Kijiji cha Mpeta mkoani Kigoma juu ya tuhuma za kutoa taarifa ya mapigano ya askari wa Jeshi la Porini na wakulima wa eneo hilo.
Sengwe ambaye ni mkazi wa Kigoma alitoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Upande wa Utetezi, Jebra Kambole, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ambaye ameieleza mahakama hiyo kuwa alipata taarifa kupitia pahali pa kupumzikia kutoka kwa mwananchi aliyetoka Kijiji cha Mpeta kuhusu mapambano ya jamii ya wakulima na polisi.
Sengwe amedai kwamba baada ya kupata taarifa za mapambano hayo aliziwakilisha kwa baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Kigoma akiwemo Hasna Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Zitto Mbunge wa Kigoma Mjini kuwa polisi wanawatoa wakulima kwa kutumia nguvu na kwamba kuna mapambano kati ya wakulima na polisi.
Amedai kuwa baada ya taarifa hiyo, Zitto alifanya mkutano wa vyombo vya habari akiiomba Serikali ifanye uchunguzi ili kutambua kilichokuwa kikiendelea huku Mbunge Hasna akiwasilisha suala hilo bungeni.
Wakati huohuo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, amemhoji shahidi huyo kuhusu uelewa wake juu ya kesi aliyokuja kuitolea ushahidi ndipo alipojibu kuwa Zitto ameshtakiwa kwa kosa la kuwasema watu wa Mpeta.
Katuga amemuuliza shahidi huyo nani aliyemuita mahakamani hapo akadai kuwa amepigiwa simu na Zitto Kabwe kuombwa afike kuieleza mahakama anachokijua kwa kile alichomwambia kuhusu mapigano ya Mpeta.
Alipoulizwa kuhusu kwenda Mpeta kwa ajili ya kujiridhisha tukio hilo amejibu kuwa hakuweza kwenda kwa wakati huo kwa kuwa palikuwa hapaingiliki. Wakili Katuga amemuuliza shahidi huyo kama kulitokea vurugu baada ya mkutano wa Zitto akajibu kuwa hapakuwa na vurugu yoyote.
Awali shahidi wa pili kwenye kesi hiyo, Shabani Ally, ambaye ni mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Kigoma Kusini, ameieleza mahakama hiyo kuwa yeye alishuhudia majeruhi wanne kwenye mapambano kati ya wakulima na Pplisi ambao walifikishwa kwenye kituo cha afya Nguruka.
Hakimu Shahidi ameahirisha shauri hilo mpaka kesho Ijumaa, Machi 20, 2020, asubuhi.
View this post on Instagram
