
KIUNGO Mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman ‘Sheva’ anatarajiwa kuanza mazoezi ya kunyonga baiskeli kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kurudi rasmi uwanjani akitokea kwenye majeraha. Sheva ameweka wazi kwamba mazoezi hayo ya wiki mbili yatamfanya atarudi katika ubora wake uleule ambao alikuwa nao kabla ya kupata majeraha hayo.
Sheva ambaye alifunga mabao sita kwenye ligi, amekaa nje ya uwanja tangu Desemba, mwaka jana baada ya kupata majeraha ya mfupa mdogo katika mguu wa kulia akiwa na kikosi cha Taifa Stars.
Kiungo huyo ameliambia Spoti Xtra, kuwa: “Kwa sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri ambapo madaktari wameniambia nifanye mazoezi ya kunyonga baiskeli kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kurudi uwanjani, zoezi hilo nitalifanya kwa wiki mbili sambamba na mazoezi mengine madogomadogo.
“Nikimaliza kwa muda huo basi nitarejea uwanjani na mashabiki watafurahi kwa sababu wameonyesha imani kubwa kwangu.” Wakati huohuo, Daktari wa Simba, Yassin Gembe, amesema: “Hali ya Miraji imeimarika na tayari ameanza mazoezi mepesi ya kujiweka fiti kabla ya kuruhusiwa kuungana na wenzake.
Kwa sasa tunajitahidi kuchukua tahadhari zote ili asipate majeraha mengine wakati huu akiwa anakaribia kupona kabisa.”
STORI: JOEL THOMAS NA SAID ALLY