×

Tito Magoti Ahofia Corona Gerezani “Mrundikano ni Mkubwa” – Video

Mshtakiwa Tito Magoti anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanajawa na hofu kubwa kutokana na usalama wa afya zao kutokana na msongamano mkubwa magerezani.

 

Tito ambaye ni mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadam nchini (LHRC) amewasilisha hayo akiwa katika Gerezani Segerea kupitia njia ya video mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ambapo amedai kuwa mahali kwingine msongamano umezuiliwa lakini wao bado wanaishi kwa hofu na kuhisi kusahaulika katika jitihada za kitaifa za kujikinga na gonjwa la corona.

 

Magoti ameongeza kuwa, ni siku ya 14 tangu ahirisho lililopita lakini hawajawasiliana na mawakili wao wala kujua hali ya familia zao na hivyo kujisikia kutengwa na hivyo kuomba mahakama kuangalia suala hilo kisheria kuona uwezekano wa kuwaondoa katika hali hiyo ya kusahaulika.

 

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai kuwa tangu kutangazwa rasmi kwa ugonjwa wa homa ya Corona Tanzania, Serikali ilitangaza kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ikiwemo kupunguza msongamano.

 

Wankyo amedai kuwa, washtakiwa hawajabaguliwa bali ni tahadhari zilizochukuliwa na gereza za kudhibiti wageni na hakuna nia mbaya ya kuwanyima haki hiyo.

 

Akipinga hoja hiyo, Wakili wa Utetezi Fulgence Masawe amedai kuwa msongamano mkubwa gerezani ni kubebesha Gereza lawama ambazo sio zao kwani mrundikano wa mahabusu ni tatizo linalotengenezwa na kudai kuwa suala la hofu mtu hawezi kumsemea mwengine hivyo ameomba jamuhuri iondoe shauri hilo na kulirudisha baada ya upelelezi kukamilika.

 

Wankyo amejibu hoja hiyo kudai kuwa, suala la kuondoa shauri mahakamani hapo upande wa mashtaka hauko kwenye nafasi hiyo kwani lipo kwenye hatua ya upelelezi na hivyo kuomba upande wa utetezi kuwa wavumilivu.

 

Baada ya hoja hizo, Hakimu mtega amewataka mahabusu wote kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kufuata miongozo ya kujikinga kama ilivyotolewa na serikali. Kesi imehairishwa hadi Aprili 15, mwaka huu ambapo watuhumiwa watabaki gerezani.

Leave a Comment