KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, raia wa Ubelgiji, amewaagiza mabosi wa timu hiyo kuwa wanatakiwa kumalizana na wachezaji wote aliopendekeza wasajiliwe kimyakimya kutokana na kuhofia kuvurugiwa usajili wake na wapinzani wao, Simba.
Kocha huyo ametoa maagizo hayo kwa viongozi hao baada ya kuona baadhi ya nyota ambao walikuwa wanatakiwa na klabu hiyo wapinzani wao kuwaingilia na kuwapata kabla yao.
Mbelgiji huyo ametoa maagizo hayo baada ya usajili wa dirisha dogo Yanga kumkosa winga Luis Jose Miquissone ambaye alisajiliwa na Simba licha ya Yanga kuzungumza naye awali.
Habari ambazo Championi Jumatatu limezipata ni kuwa kocha huyo tayari ameshawaambia baadhi ya viongozi juu ya wachezaji wa Bongo aliowaona kuanza kufuatilia mikataba yao lakini kwa siri kuogopa kuingiliwa na Simba.
“Kocha kuna wachezaji tayari ameshawapendekeza waanze kufuatiliwa mikataba yao, hasa kwa wale ambao wapo hapa nyumbani.
“Zoezi hilo limeshaanza lakini linafanyika kwa siri sana, hatutaki kuwataja kwa sababu kocha hataki kuona wachezaji wake wanasajiliwa na Simba kama ilivyokuwa kwa wengine.
“Hivyo kinachoendelea ni wachezaji hao wameshafuatwa lakini kwa sharti la kwamba hakuna kumtaja hata mmoja ambaye atasajiliwa kwa sababu tukifanya hivyo wenzetu Simba wanatuingilia na kuwasajili wao,” kilisema chanzo hicho.
Championi Jumatatu lilimtafuta Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ambaye alisema: “Kweli usajili wetu kwa safari hii utakuwa wa kimyakimya kwa sababu wenzetu hao wamekuwa wanawasajili wachezaji ambao sisi tumekuwa tukiwataka.”
SAID ALLY
Dar es Salaam
