MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Japhari Kibaya, amesema kuwa yupo tayari kutua Simba kama uongozi wa timu hiyo kweli unahitaji huduma yake.
Kibaya ambaye amekuwa mshambuliaji tegemeo wa Mtibwa kwa misimu miwili mfululizo, amesema mkataba wake na klabu hiyo unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo atakuwa huru kwenda klabu nyingine itakayomhitaji.
Inaelezwa kuwa Simba ipo katika mchakato wa kumsajili mshambuliaji mmoja mzawa, ambaye atakuja kuwa mbadala wa John Bocco na Meddie Kagere pale ambapo wanapata dharura au majeraha na wanamtazama Kibaya kama mchezaji sahihi katika eneo hilo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kibaya amesema kuwa yeye ni mchezaji ambaye anaweza kucheza katika timu yoyote itakayomhitaji, huku akiongeza kuwa tetesi za kutakiwa na Simba amezisikia na yupo tayari kwenda kujiunga na klabu hiyo kama itahitaji huduma yake.
“Ni kweli kuna tetesi tu nazisikia hata mimi kuwa Simba inanihitaji, sina shaka kwa kuwa mpira ndio kazi yangu na isitoshe mwisho wa msimu huu namaliza kandarasi yangu na Mtibwa, kwa hiyo kama kweli viongozi wanahitaji huduma yangu nipo tayari kwenda bila shida yoyote,” alisema Kibaya ambaye amefunga mabao 7 kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Issa Liponda, Dar es Salaam
