BAADA ya wapenzi na mashabiki wa Simba katika siku za hivi karibuni kutoridhishwa na uwezo wa safu yao ya ulinzi, hatimaye uongozi wa timu hiyo umeanza kulifanyia kazi suala hilo.
Uongozi unadaiwa kuwa katika mazungumzo na beki wa kati wa timu ya Polisi Tanzania ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, mwenye uwezo wa kukabiliana na mshambuliaji yoyote yule anaitwa aIdd Mobby.
Simba imefi kia hatua hiyo baada ya kuvutiwa na uwezo wake uwanjani msimu huu akiwa na kikosi cha Polisi Tanzania, lakini pia huko nyuma alipokuwa na kikosi cha Mwadui FC pamoja na Toto Africans.
Akizungumza na Championi Jumatano, mmoja wa viongozi wa Simba alisema kuwa hali hiyo ndiyo iliyosababisha uongozi huo ufi kie hatua hiyo ya kutaka kumsajili kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu yake ya ulinzi ambayo baadhi ya nyota wake wanaonekana umri wao kuanza kuwatupa mkono, hivyo nguvu za kupambana uwanjani zimepungua.
“Mobby tayari ameshafanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wetu kwa ajili ya kumsajili kwa sababu mkataba wake na Polisi Tanzania unamalizika hivi karibuni.
“Uwezo wake mkubwa uwanjani ndiyo sababu hasa iliyosababisha tufi kie uamuzi huo, kwani anakila sifa ya kuitumikia timu ya Simba ukizingatia baadhi ya mabeki wetu umri wao umeanza kuwatupa mkono,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Mabeki ambao katika kikosi cha Simba wamekuwa wakipigiwa kelele kuhusiana na kushuka kwa uwezo wao ni Erasto Nyoni pamoja Pascal Wawa ambao pia umri wao uanaonekana kuwatupa mkono. Wawa kwa sasa ana umri wa miaka 34 wakati Nyoni kwa upande wake ana miaka 31.
Alipotafutwa Mobby ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa: “Sina cha kusema kuhusiana na hilo, kama suala hilo lipo, basi ukweli wake utajulikana.”

