JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, limewapongeza wamiliki na watumiaji wa vyombo vya usafiri jijini Dar es salaam amabo wametii amri ya serikali ya kupakia abiria kulingana na idadi ya viti vilivyopo ndani ya gari (level seat) na kusisitiza kuwa waliokaidi agizo hilo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar, leo Alhamuisi, Aprili 9, 2020, Kamanda wa Polisi Dar es salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo linaendelea kusimamia ukaaji kwenye viti tunaita ‘Level Seat’.
“Hatutaruhusu watu kuendelea kusimama kwenye mabasi na hiyo haina “excuse” kwa mabasi yaendayo mwendokasi. Ninawaasa madereva bodaboda kufuata sheria wanapoingia kati kati ya Mji kwa kuvaa Helment, kutopandisha mishkaki na kutotumia barabara za Mwendokasi na kwa watakaokiuka watachukuliwa hatua.
“Mikusanyiko kwenye fukwe za bahari wakati wa sikukuu iepukwe kwakuwa siyo ya lazima. Na ikumbukwe kwa utamaduni uliopo Dar es salaam mabasi mengi yanajaza Watoto wadogo kuelekea ufukweni hatutaruhusu magari hayo kufanya hivyo,” amesema Mambosasa.
Aidha, Kamanda Mambosasa amewataka wakazi wa jiji la Dar es salaam kuepuka kufanya uhalifu, au vurugu pamoja na kutofanya mikusanyiko isiyo ya lazima katika kipindi cha sikukuu ya Pasaka ikiwa ni jitihada za kujikinga dhidi ya virusi vya corona.
