KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amefunguka kuwa kwenye ripoti yake ya usajili ambayo amewakabidhi mabosi wa timu hiyo, ni kuwa anahitaji mshambuliaji wa kati ambaye atakuja kusaidiana na John Bocco na Meddie Kagere huku akihitaji viungo wawili wachezeshaji ambao watakuja kumpa msaada Clatous Chama.
Kocha huyo ameongeza kuwa moja ya tageti zake ni kwa nyota wa Namungo FC, Luka Kikoti ambaye yupo kwenye fomu kubwa ikiwemo kucheza vizuri kwenye mechi yao huku akiweka bayana kwamba hakuna mchezaji hata mmoja wa Yanga ambaye anaweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kocha huyo ameweka wazi kwamba anawahitaji nyota hao kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chake cha msimu huu licha ya kwamba wamekuwa na kikosi kizuri chenye wachezaji wenye viwango vikubwa.
Sven amesema kwamba anawahitaji wachezaji wa nafasi hiyo kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wanacheza maeneo ya ulinzi na mawinga hivyo kuwapata nyota hao watatu wapya itakuwa imeongeza nguvu kubwa sana kikosini kwake.
“Tuna kikosi kizuri hapa na nafi kiria tutaendelea na kila mmoja aliyepo japokuwa tutahitaji wachezaji kadhaa wapya katika kila nafasi, kuna maeneo ya kuongeza watu kwenye kikosi hiki cha sasa.
Tuna wachezaji wengi wa kulinda na mawinga, kwa hiyo ni lazima tubalansi timu, tunahitaji kuwa na mshambuliaji wa mwisho na wachezaji wawili viungo.
“Kama nilivyokuja nilikuwa nachezesha mshambuliaji mmoja kwa sababu ni Kagere (Meddie) pekee ndiye alikuwa fi ti kucheza, Bocco alikuwa mgonjwa na Miraji pia alikuwa mgonjwa pia, kwa hiyo sikuwa na namna zaidi ya kumchezesha mshambuliaji mmoja.
“Kuna kiungo wa Namungo FC wakati tulipocheza nao hapa Dar alivaa namba nane (Luka Kikoti), nilimpenda alicheza vizuri na sisi pamoja na lile bao la mbali ambalo alitufunga, lakini kuna tatizo la mchezaji kudumu kwenye kiwango.
Sijui atamaliza vipi msimu lakini siyo yeye tu hata hapa kuna wakati mwingine wanacheza vizuri kabisa mechi sita hadi nane na muda mwingine vitu vinakuwa tofauti.
“Licha ya kwamba Yanga walitufunga kwenye dabi lakini sioni hata mchezaji mmoja wa Yanga anaweza kuja na kuingia kwenye kikosi chetu cha sasa,” alisema Mbelgiji huyo.
SAID ALLY, Dar es Salaam
