Jamii imehimizwa kushirikiana kwa karibu na wasaidizi wa kisheria chini ili kuwalinda wasichana na ndoa za utotoni ambazo huchochea umaskini, maradhi na ujinga.
Meneja Programu wa kituo cha Wasaidizi wa Kisheria mkoani Shinyanga, John Shija alitoa wito huo baada ya kuingilia Kati mpango wa Familia moja mkoani hapo kudaiwa kumuoza binti yao katika umri mdogo.
“Kutokana na mkakati huu hatua za haraka zilichukuliwa ili kumnusuru binti huyu asiolewe kwa kulazimishwa akiwa katika umri mdogo na kupoteza kabisa ndoto zake za maisha,” alisema.
Ndoa za utotoni zimekuwa ni tatizo kubwa ambalo huwazulumu mabinti wadogo haki zao za msingi katika maisha. Wasaidizi wa kisheria katika kila wilaya wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana ya kuwasaidia wale wanaodhulumiwa haki zao za kisheria na pia kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria katika maeneo hayo.
Taarifa hizo za mpango wa kumuozesha binti huyo ziliwafikia watoa huduma za msaada wa kisheria na ilikuwa bahati kwani mpango huo haukuwa umefika hatua ya mbali zaidi kutaka kuolewa.
Ili kuzuia mpango huo kuendelea hatua za haraka zilichukuliwa kwa ushirikiano na raia wema katika kijiji hicho. Kituo cha PACESHI kilichukua hatua muhimu kumuelimisha baba wa binti huyo juu ya masuala ya Kisheria na haki za watoto na hasa kupata elimu.
PACESHI ni shirika la wasaidizi wa kisheria chini ya ufadhili wa Legal Services Facility (LSF), shirika linalotoa ruzuku kwa mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria Tanzania Bara na visiwani Zanzibar chini ya mradi huu zaidi ya wasaidizi wa kisheria 3700 walioko kila wilaya wameendelea kutoa msaada wa kisheria kwa jamiii.
Kwa wastani kwa mwaka wasaidizi wa kisheria hushughulikia
Katika hali hii ambapo ng’ombe watano na kiasi cha laki tatu ilikuwa vimetolewa, kituo cha PACESHI kwa kushirikiana na Wasaidizi wengine wa kisheria walibeba jukumu la kuhakikisha kuwa binti huyo haolewi katika umri mdogo bali anapata ujuzi ambao utaweka msingi katika maisha yake.
Kituo cha PACESHI kilimuwezesha binti huyo kupata nafasi ya mafunzo ya kushona nguo katika chuo cha VETA mkoani Shinyanga. Binti huyo alisema baada ya kuanza mafunzo ya ufundi kuwa yatamuwezesha kufikia ndoto zake za kuwa na maisha bora baadae.
Kituo cha PACESHI pamoja na wasaidizi wengine wa Kisheria mkoani Shinyanga walikaa pamoja na wazazi wa binti huyo na kufikia makubaliano ya kumsaidia ili aweze kupata mafunzo ya ufundi wa kushona nguo.
Zaidi ya hapo kituo cha PACESHI kiliahidi kumpatia mtaji wa kuanzia pale atakapokuwa amehitimisha mafunzo yake ili aweze kuanzisha biashara ya kushona nguo ikiwa pamoja na kununua mashine ya kushona nguo.
Kwa upande wake, Theresia Masinga, ni mwalimu wa chuo cha VETA Shinyanga alisema tangu siku ya kwanza binti huyo alipoanza mafunzo ameonyesha bidii kubwa sana na kuwa jitihada hizi ni kiashiria cha malengo aliyojiwekea katika maisha.
Binti huyo anawakilisha sehemu ndogo sana ya mabinti Wengi ambao wamekuwa wakidhulumiwa haki zao za msingi za kupata elimu.
