KWENYE playlist yako ya wakali wa Bongo Fleva, huwezi kuacha jina la dogo anayetumikia Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Mondi’.
Huyu ni Mbwana Yusuph Kilungi ‘Mbosso’ ambaye mbali na kuimba sana, ni bonge moja la mtunzi.
Mbosso ambaye amezaliwa Oktoba 3, 1991 pale kijijini kwao Kibiti mkoani Pwani, ana ngoma kibao zilizokimbiza, zinazokimbiza na zitakazokimbiza ndani na nje ya Bongo.
Mbosso anayetisha na Ngoma ya Tamba kwa sasa, alianza kusikika na Yamoto Band yapata miaka nane iliyopita akiwa na madogo wenzake; Aslay, Beka Flavour na Enock Beka.
Baada ya Yamoto Band kufa, Mbosso alirudi kijijini kwao Kibiti. Huko alidaiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu baada ya kukata tamaa na kuona wenzake wakipata mafanikio, huku yeye akiwa amebaki tu nyumbani.
Alifanya hivyo kwa muda mrefu na kila mtu akaamini biashara yake ndiyo imeisha. Lakini haijulikani Mondi alitumia jicho gani kumuona Mbosso na kumrudisha upya na kumuweka kwenye ramani ya Bongo Fleva.
Ngoma ya kwanza ya Mbosso kusikika akiwa Wasafi ni ile ya Watakubali. Alitambulishwa rasmi Wasafi Januari 29, 2018.
Hadi sasa Mbosso amesikika kwenye ngoma nyingi mno kama Nimekuzoea, Alele, Shida, Picha Yake, Hodari, Nipepee, Tamu, Shilingi, Zilipendwa, Jibebe na nyingine kibwena.
OVER THE WEEKEND imemuona na kupiga mastori mengi na Mbosso ambaye anapenda kujiita Mbosso Khan au Muhindi wa Kusini Mwenye Mapenzi Tele, ambapo amefunguka juu ya ishu kibao kuhusu muziki wake na nje ya muziki. Dondoka naye;
OVER THE WEEKEND: Bado ngoma yako ya Tamba inatrendi, unazungumziaje mapokezi yake?
MBOSSO: Namshukuru Mungu mapokezi yamekuwa makubwa mno pamoja na kwamba imekutana na janga la Corona.
OVER THE WEEKEND: Janga hili la Corona limekuathiri kiasi gani kama msanii?
MBOSSO: Vitu vingi vimekwama. Kama wasanii, Corona imetuathiri mno kwa sababu tunategemea shoo na kama unavyojua shoo ni mikusanyiko ya watu na mikusanyiko imepigwa marufuku. Kila mtu kwa imani yake, anatakiwa aendelee kumuomba Mungu ili janga hili liondoke.
OVER THE WEEKEND: Unafanya jitihada gani katika kipindi hiki cha Corona ili usishuke kimuziki?
MBOSSO: Naendelea kutunga ngoma kali na kufanya video. Naomba Corona tuichukulie kama ni changamoto tu kwenye maisha, ipo siku itapita na tutarudi tena kwa kishindo.
OVER THE WEEKEND: Mbali na muziki, unajishughulisha na nini kinachokupatia kipato nyakati kama hizi za Corona?
MBOSSO: Bado sijawa na biashara kubwa, ila kuna vitu vidogovidogo ambavyo vinaniingizia pesa na ninamshukuru Mungu kwa hilo.
OVER THE WEEKEND: Unazungumziaje hatua ya Wasafi kumsajili Zuchu na unamuona wapi baada ya miaka mitano?
MBOSSO: Zuchu ni msanii mkubwa sana. Miaka mitano ijayo ni mbali sana, mimi namzungumzia baada ya miezi sita tu, atakuwa ni mtu mwingine tofauti kwa sababu ana uwezo mkubwa, watu wazidi kuipa sapoti EP yake ili naye afikie malengo yake.
OVER THE WEEKEND: Kwa nini hufanyi kolabo na wenzako wa Wasafi kama Lava Lava na Rayvanny?
MBOSSO: Kolabo siyo ishu ya kufanya tu, ila ni kupanga ngoma sahihi ambayo mnaweza kufanya watu waone viwango, hatuwezi kufanya tu eti ili kuridhisha mashabiki. Nina imani ipo siku mipango itakuwa sawa.
OVER THE WEEKEND: Kuna kipindi ulikuwa unamposti sana mama mtoto wako, marehemu Boss Matha, ni vitu gani unavikumbuka kwake?
MBOSSO: Naomba nisilizungumzie hilo kwa sasa.
OVER THE WEEKEND: Vipi kuhusu mtoto ambaye umezaa na Boss Matha, hujapewa mpaka sasa?
MBOSSO: Pia hilo nalo naomba nisilijibu kwa sasa kama hutajali tafadhali.
OVER THE WEEKEND: Vipi kuhusu kolabo za kimataifa?
MBOSSO: Mwaka huu tayari nimefanya kolabo mbili za nje ikiwemo ile ya Ngoma ya Lavie na Tanasha, ila zote nilishirikishwa. Mipango ni mingi, lakini imeharibiwa na Corona.
OVER THE WEEKEND:Unakubalika sana mjini Mombasa na Kenya, siri ni nini na una mpango wa kwenda kuishi huko?
MBOSSO:Ni kweli ninakubalika sana Mombasa, lakini suala la kwenda kuishi huko bado sijalifikiria.
OVER THE WEEKEND:Je, ni kweli umeachana na mzazi mwenzako, Rukia?
MBOSSO: Sipo kwenye mazingira mazuri sana ya kuzungumzia masuala ya kifamilia, ningependa tuzungumzie zaidi masuala ya muziki wangu.
OVER THE WEEKEND: Una nyota ya kupendwa na watoto wa Kiarabu, unalizungumziaje suala hilo?
MBOSSO: Ni kweli, lakini hilo ni jambo la kawaida. Ukiwa mwanaume kamili lazima upate usumbufu kutoka kwa wanawake. Unaweza ukawa unauza genge tu na bado mwanamke akakupenda. Ni nyota tu, sidhani kama wananisumbua kwa nia mbaya, wananisumbua kwa sababu wanapenda staili ya maisha yangu.
OVER THE WEEKEND: Ni changamoto gani unakutana nazo kwenye muziki wako?
MBOSSO: Changamoto ni kawaida tu. Kwa upande wangu siwezi kusema nina changamoto kubwa.
OVER THE WEEKEND: Hongera kwa kufanikisha kuwajengea wazazi wako nyumba, labda unawashauri nini vijana wenzako ambao wanapata pesa, lakini hawawakumbuki wazazi wao?
MBOSSO: Nafikiri tuongeze bidii kwenye kazi zetu na tumuombe Mungu atupe mioyo ya kukumbuka wazazi na kuwasaidia ili tupate baraka zao.
OVER THE WEEKEND: Vipi kuhusu mipango yako ya kufunga ndoa, imekaaje?
MBOSSO: Sina mpango wa kuoa kwa sasa.
OVER THE WEEKEND: Una lipi la kuwaambia mashabiki wako?
MBOSSO: Tupo kwenye kipindi kigumu mno cha janga la Corona, wafuate taratibu za kujikinga zinazotolewa na wataalam wa afya.
