WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema hakuna haja ya kupandisha bei ya sukari kutokana na gonjwa la corona kwani sukari ipo ya kutosha na wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria haraka.
Majaliwa amesema hayo leo Jumatano, Aprili 22, 2020 wakati akihutubia kwenye maombi ya kitaifa dhidi ya janga la corona yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Wiki hii waumini wa Kiislamu wanaanza mfungo wa Ramadhan, hivyo natoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha vyakula muhimu vinauzwa kwa bei ya kawaida.
“Nawaagiza wakuu wa mikoa na wilaya, wafanye ukaguzi mara kwa mara kwenye masoko ili kuhakikisha bei ni ileile. Ikibainika, wanaopandisha bei ya sukari wawachukulie hatua kali.
“Hakuna sababu ya bei ya sukari kupanda, sukari ipo tena ya kutosha, ilikuwa imepungua imeagizwa na imekwishaletwa, nawaagiza wakuu wa mikoa kwamba yeyote atakayeuza sukari kwa shilingi 4,500, chukueni hatua kali dhidi yake,” amesema Majaliwa.
