×

Wabunge Watoa Sababu Za Simba Kupewa Ubingwa

 Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

BAADHI ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameshauri Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuifuta ligi msimu huu na ubingwa kuipa Simba ambayo inaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi nyingi zaidi ya timu zinazofuatia wakidai hali siyo salama kwa ligi kurejea kwa sasa.

 

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja katika kikao cha bunge juzi Alhamisi, ambapo kwa pamoja waliitaka TFF kufikiria kwa kina juu ya kuifuta ligi hiyo kutokana na janga la Corona, huku wakisema timu mbili za juu ziende kuiwakilisha nchi kimataifa.Akitoa maoni yake juu ya mwenendo wa ligi kuu nchini, Nkamia alisema:

“Nawaomba TFF, waangalie uwezekano wa kuifuta ligi na timu mbili za juu mmoja akipewa ubingwa na mwingine akipewa tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya FA, kwa sababu hali ya sasa siyo salama kwa ligi hiyo kuendelea kutokana na janga la Corona ni vyema wakatumia busara hiyo.

 

”Upande wa Ngeleja naye aliunga mkono kauli ya Nkamia kwa kusema: “Msimbazi wapewe kombe lao na hao Utopolo wasubiri tu msimu ujao wajipange upya, kwa sababu kwa hali ilivyo hakuna namna ya kuweza kuizuia Simba isiwe bingwa, kwa sababu wanaongoza ligi kwa pointi nyingi sana, nafikiri TFF, ni vyema wakatumia busara hiyo ya kumtangaza bingwa tu.

 

”Wakati wabunge hao wakitoa maoni hayo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Almas Kasongo, aliwahi kunukuliwa akisema: “Kwa sasa hatuna jibu kamili la kusema lini ligi itarejea, sababu hatujui hali hii itafikia ukomo siku gani, kikubwa tunasikilizia taarifa kutoka serikalini ili na sisi tujue tunafanyaje ili kuweza kumalizia michezo iliyobaki.”

 

Simba wapo kieleni na pointi zao 71, baada ya michezo 28, huku Azam FC akifuatia katika nafasi ya pili na pointi 54, Yanga katika nafasi ya tatu na alama 51 wakifuatiwa na Namungo FC katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 50

Leave a Comment