MDOGOMDOGO sasa vita inataka kuhama kutoka kwa mabosi kwenda kwa wasanii wao ambapo msanii wa Bongo Fleva aliyesainiwa kwenye Lebo ya Konde Gang Music Worldwide chini ya Harmonize, Ibrah anadaiwa kufuata nyayo za yule aliyesainiwa Wasafi chini ya Mondi, Zuchu.
Baada ya Zuchu kuachia EP (albam fupi) yake ya IAM ZUCHU, Ibrah naye yupo mbioni kuachia ya kwake inayokwenda kwa jina la STEPS. Wakati ile ya Zuchu ina nyimbo saba, ya Ibrah ina jumla ya nyimbo tano.
Ibrah ameweka wazi mipango yake hiyo ikiwa ni wiki moja tu tangu Harmo alipotambulisha kazi zake. Wakati Zuchu akikimbiza na ngoma kibao zilizoingia kwenye trending ya YouTube na mitandao mingine ya kijamii, Ibrah yeye ananyanyasa na wimbo wake wa Nimekubali.
Kwa mujibu wa Ibrah, ndani ya EP yake hiyo amewakutanisha wasanii wakubwa wawili kutoka Nigeria, Skibii na Joeboy. Pia kwenye wimbo wa mwisho Ibrah amempa shavu bosi wake kwenye ngoma iitwayo One Night Stand ambayo inapatikana ndani ya EP hiyo.
STORI: NEEMA ADRIAN, DAR
