Ligi Kuu Soka nchini Ufaransa (The Ligue 1) na Ligi Daraja la Pili (Ligue 2) zimefutwa baada ya Waziri Mkuu wa nchini hiyo kusema michezo yote itatakiwa kuendelea Septemba 2020.
Amesema kuwa, michezo yote iwe inachezwa bila mashabiki au na mashabiki haitaweza kuendelea nchini humo kabla ya Septemba mwaka huu.
Ligue 1 na Ligue 2 zilipangwa kuendelea kuchezwa Juni 17, 2020 huku Shirikisho la Soka Ulaya likiweka hadi Agosti 2, 2020 kuwa Ligi zote za ndani barani humo ziwe zimemalizika.
Shirikisho linalosimamia Ligi hizo limepanga kukutana Mei 2020 ili kujadili ni kwa namna gani msimamo wa ligi utatafsiriwa na timu zipi zitashuka daraja na zipi zitapanda daraja.
Pia, watajadili timu gani zitapata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na kama PSG inayoongoza Ligi hiyo kwa tofauti ya alama 12 hadi sasa itawazwe kuwa Bingwa.
