×

Mondi, Zari Ndoa Asilimia 100

KITENDO cha staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kusema kuwa, kwa sasa ana mawasiliano mazuri na mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, kimeibua mapya kutoka kwa wafuasi wao ambapo kwa pamoja wametamka; ‘kifuatacho ni ndoa 100%’.

 

WAFUASI MIL 16.8

Diamond au Mondi na Zari, hadi juzi Jumatatu, walikuwa na jumla ya wafuasi wapatao milioni 16.8 kwenye kurasa zao za Instagram ambapo jamaa huyo alikuwa nao milioni 9.3 huku mwanamama huyo akiwa nao milioni 7.5.

 

Katika mahojiano maalum na vituo vyake vya redio na televisheni vya Wasafi juzi, Mondi alifunguka juu ya ujumbe wa Zari kuhusiana na malezi ya watoto wao wawili; Tiffah Dangote na Prince Nillan.

Mara tu baada ya Mondi kutangaza kusaidia familia 500 kulipa kodi ya pango kufuatia janga la Corona, Zari aliibuka na kumtuhumu jamaa huyo kuwa, hana lolote kwani ameshindwa hata kuwalea wanawe na kumtelekezea yeye.

 

MONDI AMJIBU ZARI

Akizungumzia ishu hiyo, Mondi alisema; “Baada ya kuona ujumbe ule wa Zari, nilimpigia simu na kumueleza kuwa, licha ya tofauti zetu, bado ninamheshimu sana.

“Alinielewa na nadhani baada ya Corona kuisha, tutapanga namna ya kuwalea watoto wetu pamoja.

 

“Mnapokuwa mmetengana wewe na mzazi mwenzako, lazima kunakuwa na hasira. Hivyo, mtu anaweza kusema chochote ilimradi akuumize.”

Mbali na hayo, Mondi alipoulizwa juu ya suala la kuachana na mzazi mwenzake mwingine, Tanasha Donna, alisema;

 

“Mimi na Tanasha hatujatengana kwa sababu ya kufumaniana, bali kuna sababu ambazo yeye binafsi aliniambia na kusema anahitaji nafasi, hivyo niliheshimu maamuzi yake.

“Nilipanga kumuoa Tanasha 100% kwa sababu ni mwanamke ambaye nilitulia sana wakati nipo naye, niliweka ujana wangu pembeni.”

 

ATAKAYEINGIA KUMI NA NANE

Kuhusu kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa sasa, Mondi alisema; “Kwa sasa sina mpenzi na sitaki, lakini atakayeingia kwenye kumi na nane nitamuoa hapohapo.”

 

AREJESHWA KWA ZARI

Kufuatia maelezo yake hayo, ndipo wafuasi wa Mondi na Zari wakaibuka na kusema kuwa, bora jamaa huyo arejee kwa Zari na kujihakikishia kufunga naye ndoa kwa asilimia mia moja.

Mashabiki hao walifunguka kuwa, katika kipindi ambacho Mondi hana mpenzi kama alivyosema, ni vyema akatafakari mambo na kurejea kwa Zari ambaye ana vigezo vyote.

 

“Pamoja na kwamba Zari ni mama wa watoto watano, lakini bado anaita na ana msisimko wa aina yake tofauti na wanawake wengine aliowahi kuwa nao.

“Hakuna mwanaume anayependa kukaa na mwanamke asiyekuwa na msisimko wa kimapenzi.

 

“Hebu fikiria Diamond alipokuwa na Zari walivyokuwa wanapendezeana, hata sisi tulikuwa tunapata msisimko.

“Hata Zari anang’aa, anameremeta, mwanamke yupo bomba, ukikaa karibu yake tu utagundua kwamba umekaa na mwanamke mwenye mvuto ambaye kila wakati atakufanya kuwa bize kumwangalia.

 

“Zari anajitambua, haendeshwi na ustaa pamoja na kwamba ni staa mkubwa Afrika Mashariki na hata Afrika kwa ujumla. Ni mwanamke mwenye hekima na busara sana. Si mzungumzaji kivile na huwa anapenda kufanya vitu kwa vitendo kuliko maneno.

 

“Zari anajiamini sana, anajua kuona fursa, si mwanamke tegemezi na ni mama bora kwenye familia yake.

“Diamond hajawahi kupata mwanamke mwenye vigezo vyote kama Zari.”

Ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya Mondi kurejeshwa kwa Zari.

 

Katikati ya mjadala huo, gazeti hili lilizungumza na mtu wa ndani ya familia ya Mondi ambaye alisema kuwa, licha ya jamaa huyo kutofautiana na Zari kwa muda mrefu, lakini wapo baadhi ya watu kwenye familia hiyo ambao wamekuwa wakiwasiliana na mwanamama huyo mara kwa mara huku pia wakitamani arejee kwenye himaya yake.

 

ZARI AKIRI MONDI KUMMISI

Wiki mbili zilizopita, naye Zari alikiri kupokea ujumbe kutoka kwa mpenzi wake huyo wa zamani akimwambia kuwa amemmisi.

 

Zari ambaye ni raia wa nchini Uganda mwenye maskani yake Durban, Afrika Kusini, alimwagana na Mondi Februari 14, 2018 baada ya mrembo huyo aliyezaa naye watoto wawili, Tiffah Dangote na Nillan kuandika bonge la waraka akimtuhumu Mondi kuwa amekuwa na vitendo vinavyomvunjia heshima na hadhi yake katika jamii.

 

Tangu wamwagane, Mondi hakuwa na mawasiliano mazuri na mama watoto wake huyo hadi akaanzisha uhusiano mpya na Tanasha ambaye naye wamekuja kumwagana akiwa amezaa naye mtoto mmoja wa kiume, Naseeb Junior, lakini sasa moshi mweupe unaonekana kati ya Mondi na Zari.

STORI | Sifael Paul, Risasi

Leave a Comment