WIKI hii imekuwa na matukio mengi hususan ya misiba kwenye maeneo mbalimbali! Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi, amina.
Kwenye ulimwengu wa burudani, gumzo kubwa lilikuwa ni la mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi kuzungumza ‘live’ kwenye runinga yake ya Wasafi kuhusu masuala mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine, alimzungumzia mzazi mwenzake Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.
Baada ya kupita muda mrefu bila mawasiliano, kwa mara ya kwanza Mondi alithibitisha kuanza kuongea na Zari, angalau mazungumzo yao yanaleta picha mpya ya kulea watoto wao kwa pamoja.
“Zari alimaindi niliposema nachangia kodi za nyumba kwa watu 500, ikabidi nimpigie nikamuweka sawa. Akaeleza dukuduku lake, na mimi nikamuelewesha, tukawekana sawa basi naamini kila kitu kikawa sawa na naamini baada ya Ramadhani, nadhani sasa tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya mimi na yeye kulea watoto wetu kwa pamoja,” alisema Mondi.
Kwenye mahojiano hayo, Mondi pia aliwazungumzia wapenzi wake wengine akiwemo Tanasha Donna ambapo alidai kuwa, alikuwa tayari kumuoa lakini hata hivyo, Tanasha alionekana kutokuwa tayari, hivyo wakafikia uamuzi wa kupeana nafasi ya kila mmoja kufanya mambo yake.
Kama hiyo haitoshi kwenye mahojiano hayo, Mondi pia alitumia nafasi hiyo kuwaeleza mashabiki wake kuwa, amenunua hoteli ya kisasa iliyopo maeneo ya Mikocheni B jijini Dar na kwamba, ana mpango wa kuikarabati iwe ya kisasa zaidi.
“Kwa wakati huu ambao bado sijaanza ukarabati, nipo tayari kuitoa kwa Serikali ili itumike kama eneo la kuhifadhia watu wanaohisiwa au kuwa na maambukizi ya Corona,” alisema Diamond.
STORI: MWANDISHI WETU, RISASI
