WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amelieleza Bunge kuwa kwa mujibu wa Serikali ya Zambia, nchi hiyo haijafunga mpaka wake na Tanzania katika eneo la Nakonde huko Tunduma.
Amesema; “Nataka niwaambie, Zambia haijafunga mpaka na Tanzania. Ninayo barua kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Joseph Malanji ambaye Mungu amemjalia kujua lugha nyingi. Hapa #Tanzania anazungumza Kinyakyusa, Kinyiha na Kinyamwanga na nimezungumza naye kwa Kiswahili.”
Akisoma barua aliyotumiwa na Waziri huyo wa #Zambia, imeeleza “Zambia imeamua kwa muda kuzuia usafirishaji wa huduma na bidhaa katika mpaka wa Nakonde kwa muda wa awali wa siku 5 kutokana na idadi kubwa ya Wagonjwa wa #COVID19 waliokuwa wakipatikana eneo hilo.”
Barua hiyo imeeleza kuwa lengo ni kuruhusu kufanyika kwa upimaji mkubwa, ufuatialiji wa watu na kuhakikisha hatua zinawekwa ili kuzuia kusambaaji wa #CoronaVirus kutoka Nakonde kwenda sehemu nyingine za Zambia.
Aidha, barua hiyo imeeleza kuwa timu ya Wataalum kutoka Zambia iko tayari kukutana na timu ya Wataalam kutoka Tanzania ili kuweka sawa mambo katika eneo hilo na kuhakikisha shughuli zinaendelea na kamwe Tanzania haitaruhusu maadui kutaka kuivuruga Jumuiya ya Afrika Mashariki.
