×

Kazi Imeisha, Bosi GSM: Majembe haya mali ya Yanga

KAULI pekee inayopaswa kutumika kwa Wanayanga sasa ni hii ya mambo ni moto, hasa baada ya Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Eng Hersi Said, kuweka wazi kuwa takriban wachezaji wote wa kimataifa na ndani ambao kocha wao Luc Eymael anawahitaji msimu ujao, wameshamalizana nao na kinachosubiriwa ni dirisha kufunguliwa.

 

Kwa sasa ligi zimesimama kwa muda kutokana na janga la Virusi vya Corona lakini timu nyingi zimeshaanza mawindo ya kusajili wachezaji wao haraka ili kuepuka upinzani pindi madirisha yatakapofunguliwa.

 

Hapa Bongo, Yanga imekuwa ikihusishwa na wachezaji kadhaa wa kimataifa kama winga wa AS Vita ya DR Congo, Tuisila Kisinda, kiungo mkabaji Ally Niyonzima raia wa Rwanda, anayekipiga Rayon Sports ya nchini humo, pia kuna Heritier Makambo anayekipiga Horoya AC ya nchini Guinea na wengineo.

Kwa upande wa wachezaji wa ndani kuna straika wa Namungo FC, Reliants Lusajo, beki wa kati wa Coastal Union ya Tanga, Bakari Mwamnyeto sambamba na kiungo wa kati wa Polisi Tanzania, Baraka Majogoro na mlinzi wa kushoto, Yassin Mohamed.

 

Sasa Championi Jumamosi, lilimtafuta Injinia Hersi ili aweze kuweka wazi mambo haya ya usajili ambapo bila kificho aliwataarifu wasomaji wa gazeti hili kuwa ni kweli kabisa.

 

Hersi alisema takriban nyota wote wa nje na ndani ya nchi ambao kocha Eymael aliwataja kwenye ripoti yake wameshamalizana nao kwa kufanya mazungumzo na kilichosalia kwa sasa ni siku ya kuwatangaza pekee.

“Tunamshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kufanikisha mambo yetu ya usajili, takriban yote kwa muda mfupi, kikubwa tunamuomba aendelee kuwajaalia uzima wachezaji wetu wote ambao tumeshafanya nao mazungumzo ili wamalize mikataba yao wakiwa na afya njema.

 

“Tuendelee kusubiria muda wa dirisha kufunguliwa ili wachezaji hao waweze kuja na kutangazwa kisha tukamilishe suala la uboreshaji wa kikosi kama matarajio ya kocha wetu yalivyo.

Lusajo

“Wengi wamekuwa wakiniuliza sana kuhusu uwepo wa Makambo msimu ujao, kubwa niwatoe wasiwasi tu kwamba Makambo ni kati ya wachezaji wetu ambao wapo kwenye malengo ya msimu ujao lakini hata wengine wote waliotajwa zaidi nikimaanisha wale wa kutoka Congo na hata Rwanda,” alisema Eng Hersi.

Stori: Musa Mateja,Dar es Salaam

 

Leave a Comment