
DAR: Wakati janga la maambukizi ya Virusi vya Corona likiendelea kutikisa nchi 212 duniani, idadi kubwa ya wanawake inatarajiwa kukosa huduma za uzazi wa mpango wa kisasa na kusababisha mimba milioni saba kutokana na nchi nyingi kusisitiza amri ya kuendelea kusalia nyumbani.
Pia wanawake wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia katika miezi ijayo iwapo amri ya kusalia ndani (lockdown) itaendelea katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Kwa mujibu wa takwimu za utafiti huo zilizotolewa Aprili, mwaka huu na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA), wanawake milioni 47 katika nchi 114 wataathirika kutokana na janga hilo.
Utafiti huo uliangazia kiwango kikubwa cha athari za Ugonjwa wa COVID-19 kwa wanawake katika kipindi hiki ambacho mifumo ya afya inazidiwa kuhudumia wagonjwa wa Corona.
Pia iliangazia vituo vya afya kufungwa au kutoa huduma chache kwa wanawake na wasichana na wengine kukwepa kwenda hospitalini kupata huduma kwa kuhofia kuambukizwa Corona.
Pia kudorora kwa mnyororo wa usambazaji na ununuzi ulimwenguni umeelezwa kusababisha uhaba wa dawa za mpango wa uzazi.
Akifafanua kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Dk Natalia Kanem, alisema; “Takwimu hizi mpya zinaonesha athari ya COVID-19 linavyoweza kuathiri wanawake na wasichana duniani.
“Ugonjwa huu unazidisha kukosekana kwa usawa na mamilioni ya wanawake na wasichana sasa wako hatarini kupoteza uwezo wa kupanga familia zao na kulinda miili yao na afya zao. Afya ya uzazi na haki za wanawake lazima zilindwe kwa gharama yoyote. Huduma lazima ziendelee; vifaa lazima vitolewe na walio hatarini lazima walindwe na kuungwa mkono,” alisema.
MAKISIO YA TAKWIMU
Dk Natalia anasema wanawake milioni 47 katika nchi 114 zenye kipato cha chini na cha kati, wanaweza kukosa huduma za uzazi wa mpango na ujauzito milioni saba usiopangwa unatarajiwa kutokea ikiwa amri ya kuendelea kusalia nyumbani itaendelea kwa miezi sita na kukatokea usumbufu mkubwa kwa huduma za afya.
Anasema kwa kila miezi mitatu ya kuendelea kubaki nyumbani itakayoongezeka, wanawake milioni mbili wanaweza kushindwa kutumia uzazi wa mpango.
“Visa milioni 31 vya ziada vya unyanyasaji wa kijinsia vinaweza kutarajiwa kutokea ikiwa amri ya kuendelea kubaki nyumbani itaendelea kwa angalau miezi sita. Kwa kila miezi mitatu ya watu kubaki nyumbani, visa vya ziada milioni 15 vya unyanyasaji wa kijinsia vinatarajiwa.
“Kwa sababu ya kuvurugika kwa program za kuzuia ukeketaji kutokana na kujikita katika kupambana na COVID-19, visa milioni mbili vya ukeketaji vinaweza kutokea katika muongo mwingine ujao ambao ungeweza kuwa visa hivyo vimefutika,” amesema.
Amesema COVID-19 itakwamisha juhudi za kumaliza ndoa za utotoni, pengine kusababisha ndoa za watoto milioni 13 kati ya mwaka huu 2020 na 2030, matukio ambayo yangeweza yametokomezwa.
WATOTO MILIONI 116 KUZALIWA MIEZI 9
Aidha, mbali na mimba zisizotarajiwa milioni saba, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, (UNICEF) pia limeongeza kuwa inakadiriwa kuwa watoto milioni 116 watakuwa wamezaliwa wiki 40 tangu Corona itangazwe kuwa janga la kimataifa Machi 11, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore alisema watoto hao watazaliwa katika kipindi cha machungu mapya ikiwemo hatua za kuzuia kuchangamana.
Alisema pia ni kipindi ambacho vituo vya afya kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma, ukosefu wa vifaa vya matibabu, uhaba wa wahudumu wa afya wenye stadi za kutosha kwa kuwa wengi wanahudumia wagonjwa wa Corona sambamba na amri za kutotembea hovyo.
Alisema ni vigumu kufikiria ni kwa jinsi gani Corona imeathiri uzazi hivyo UNICEF inaonya; “Hatua za kuzuia watu kutoka majumbani zinaweza kuvuruga huduma za afya za kuokoa maisha kama vile huduma za kujifungua na hivyo kuwaweka mamilioni ya wajawazito na watoto wao hatarini.”
NCHI ZITAKAZOKUWA NA WATOTO WENGI
UNICEF inasema kuwa nchi zinazotarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto miezi tisa baada ya COVID-19 kutambuliwa kuwa ni janga ni pamoja na India (watoto milioni 20.1), China (watoto milioni 13.5), Nigeria (watoto milioni 6.4) huku Pakistan ikitarajia watoto milioni 5 na Indonesia watoto milioni 4.
Shirika hilo linasema kuwa idadi kubwa ya mataifa hayo tayari yana viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga, hata kabla ya janga la COVID-19 na hivyo viwango hivyo vinaweza kuongezeka wakati huu wa Corona.
Marekani nayo ambayo imeathiriwa na janga la Corona inatarajia zaidi ya watoto milioni 3.3 kuzaliwa kati ya Machi 11 hadi Desemba ambapo mamlaka za Jimbo la New York, zinaangalia mbinu ya kuweka vituo vya kujifungulia kwa kuwa wajawazito wengi wanahofia kwenda kujifungulia hospitalini.
UNICEF inaonya kuwa ingawa ushahidi unaonesha kuwa wajawazito hawaathiriwi zaidi na COVID-19 kama ilivyo kwa watu wengine, Serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa bado wanapata huduma za kabla ya kujifungua, za kujifungua na baada ya kujifungua.
Stori: GABRIEL MUNSHI, Ijumaa