
TAASISI ya Mohammed Dewji (Mo Dewji Foundation) na Timu ya Mpira wa Miguu ya Simba wamekabidhi vituo vya kuosha mikono, sabuni pamoja na vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) lengo ikiwa ni kusaidia kudhibiti maambukizi ya Covid 19.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Mo Dewji Foundation Bi. Barbara Gonzalez amesema kuwa ujenzi wa vituo hivyo ni mwanzo wa zoezi ambalo litaendelea hivi karibuni katika hospitali nyingine kama Mloganzila, Mwananyamala, Temeke na Amana.

“Tunatumia nafasi hii kuwashukuru uongozi wa hospitali zote tatu na kila mmoja wenu ambaye alishiriki kufanikisha kazi hii pamoja na kuwepo kwa changamoto ugonjwa wa Codiv19, ”amesema Barbara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Timu ya Simba, Senzo Mazingiza, amesema kuwa wanatambua mchango mkubwa sana unaofanywa na watumishi wa sekta nzima ya afya na hivyo wameona wachangie sabuni pamoja na vitakasa mikono.

Wakipokea msaada huo Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Hedwiga Swai, Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Samuel Swai na Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa Huduma za Afya ya Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Tulizo Shemu wameshukuru msaada huo kwa kuwa utasaidia kupunguza kazi ya usimamizi wa kuosha mikono ambayo mwanzo ilibidi ifanyike na walinzi katika milango mikuu na milango ya kuingia majengo yote ya hospitali.