
UMATI mkubwa wa abiria Bandari ya Dar es Salaam wameonyesha masikitiko makubwa baada ya boti ya Zanzibar 1 ya Kampuni ya Zanzibar Fast Ferry ya Unguja, kushindwa kufanya safari zake.
Umati huo zaidi ya watu 400 waliokwisha kata tiketi zao kwa ajili ya kuondoka na boti hiyo majira ya saa nane mchana, walipigwa na butwaa baada ya kutangaziwa kutofika kwa boti yao. Hali hiyo ilileta tafrani kwa abiria hata hivyo baadae uongozi uliamua kurejesha nauli zao.
“Boti hakuna leo. Wote walio na tiketi watarejeshewa nauli zao,” alisikika mmoja wa maafisa wa boti hiyo. Hata baadhi ya abiria walilalamikia kitendo hicho kwa kutojulishwa mapema licha ya kujua tatizo.
“Boti toka asubuhi haijafika hapa Dar. Lakini walishindwa tu kuwaambia ukweli abiria huu ni uhuni na maendeleo hayatafikiwa kwa hali hii” alisikika mmoja wa abiria.
Abiria mwingine alijitambulisha kwa jina la Salum Said alisema kwa hali hii imewafanya kutokuwa na imani na boti hiyo kwani imepotezea watu muda wao.
“Wametupotezea muda na hii imeanza hivi italeta matatizo zaidi huko mbeleni. Kama kuna kitu kipo baina ya hii biashara ya usafirishaji baharini basi kuna shida,” alisema Salum said.
Aidha, kufuatia hali hiyo, upande wa usafirishaji wa boti za Azam, wao wameweza kuuza tiketi zao kwa bei ya juu baada ya zile za daraja la tatu ‘Economy’ kujaa na kubakiwa na tiketi za daraja la kwanza na la pili pamoja na VIP.
Baadhi ya abiria wameonekana kulalamikia ukubwa wa bei hiyo kwa kudai kuwa wamekomolewa. Hata hivyo mwandishi wa habari hizi amewatafuta viongozi wa boti ya Zanzibar One, ambapo simu zoa ziliita bila majibu.
Katika habari zisizo rasmi kutoka visiwani Zanzibar zinaeleza kuwa kuna suala la hujuma baina ya kampuni hiyo na wapinzani wake katika usafirishaji wa baharini. Lakini pia habari zingine zinaeleza kuwa, abiria wengine walikwama kufanya safaru kutoka Unguja kuja Dar kwa boti hiyo ya Zanzibar One.
NA ANDREW CHALE