
RAIS wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, leo Mei 30, 2020 ameelezea furaha yake kwa uamuzi wa Rais wa Awamu ya Tano Dkt John Magufuli, aliyewatunuku marais wanne wastaafu kila mmoja ndege aina ya tausi 25 kwa ajili ya kwenda kupamba makazi yao.
Ametoa shukurani hizo leo Mei 30, 2020, jijini Dodoma, wakati wa zoezi la kukabidhiwa ndege hao ambazo zilikwenda sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya kujenga ofisi za Ikulu huko Chamwimno, Dodoma.
Zawadi hizo zilitolewa katika makabidhiano maalum yaliyofanywa na Rais Magufuli kwa Mama Maria Nyerere, mjane wa Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere akiwakilisha nafasi ya kiongozi huyo wa kwanza wa taifa hili; na marais wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
“Mimi nikiwa ndiye mdogo, nasema kwa niaba ya wazee hawa kwamba tunatoa shukurani kwa moyo wako wa upendo kwa kutupatia hawa ndege. Tulikuwa tunawatamani lakini ukitoka nao, ukafika nao Msoga, watu watasema umepora… Pia nakupongeza kwa maamuzi ya kuleta incubator…” amesema Kikwete.
Awali, Rais Magufuli aliwapongeza marais wote wastaafu walioshiriki kuwatunza tausi hao wakiwa ikulu.