
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel, ameagiza kuondolewa kwa safu ya uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru inayoongozwa na Mganga Mfawidhi, Dkt. Shafii Msechu, ikiwa ni sehemu ya maboresho katika sekta ya afya.
Ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara katika hospitali hiyo na kuzungumza na timu ya uendeshaji wa huduma za Afya ya Mkoa ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Wedson Sichalwe katika ofisi za Mganga Mkuu wa Mkoa huyo jijini Arusha.
“Tumeona kwamba, Hospitali ya Mount Meru inahitaji mabadiliko makubwa sana ya kiuongozi, kwa kushirikiana na mamlaka husika, yafanyike haraka sana, kwa sababu kuna mambo ya msingi sana yanayogusa jamii ambayo yanatakiwa kufanywa kwa ustadi wa hali ya juu,” alisema Dkt. Mollel.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwenye Sekta ya Afya, katika kuboresha miundombinu na huduma za afya zinazotolewa ili kuwasaidia wananchi wa vipato vya chini kupata huduma bora na nafuu bila wasi wasi.
“Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kwenye eneo la Afya. Serikali imekuwa ikileta miundombinu mingi sana kwenye eneo la Afya, fedha ambazo Serikali imezileta kwenye eneo la afya zinatakiwa matokeo hizo fedha yamguse mwananchi wa kawaida,” alisema.
Alisisitiza kuwa, pale ambapo fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya maboresho ya huduma za afya na miundombinu hazimgusi mwananchi wa kipato cha chini, ni lazima Serikali itafanya mabadiliko ili kuboresha sekta hiyo kutoa huduma bora na nafuu kwa wananchi.
Naye Dkt. Wedson Sichalwe amesema kuwa, Serikali imeboresha miundombinu katika Sekta ya Afya na utoaji huduma ikiwemo hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, ili kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma bora na nafuu.
“Mpaka sasa kazi ambayo imefanywa na Serikali ya kuboresha miundombinu ya Sekta ya Afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, katika vituo vyetu imeboreshwa, miongozo ipo, kwahiyo shida kubwa ipo katika usimamizi na ndio eneo kubwa ambalo tumeagizwa” alisema.
Aidha, amepokea agizo la usimamizi mzuri wa Sekta ya Afya katika Mkoa wa Arusha na Halmashauri zake lililotolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mbali na hayo, amesema imeendelea kutoa elimu ya mafunzo kwa watu 360 wanaojihusisha na masuala ya utalii, lengo ni kuhakikisha kuwa wanawapokea vizuri watalii na kuchukua hatua zinazostahili pindi shida yoyote inapojitokeza.
Na WAMJW- ARUSHA