×

Kisa Mtoto… Mke wa Mtu Akiona!

AMA kweli Uswahilini kuna vituko. Amina Said ambaye ni mke wa mtu, mkazi wa Buza Kwarurenge, Temeke, Dar es Salaam, amekiona cha moto, kisa mtoto! Tulia uhabarishwe.

 

Cha moto chenyewe ni “kipigo” na msukosuko wa kufa mtu kutoka kwa majirani zake ambao walidai kuchoshwa na tabia za mwanamke huyo kumfanyia ukatili mtoto wa miaka minne aliyekabidhiwa aishi naye.

 

Tukio hilo limetokea Jumapili iliyopita ambapo majirani hao walikinukisha kiasi cha kufunga mtaa na kuwafanya polisi kutia timu kumuokoa mtuhumiwa.

 

AFISA JAMII ANENA

Akizungumza na mwandishi wetu, Mhudumu wa Jamii Kitengo cha Watoto wa maeneo hayo, Amini Nyamrasa alisema:

“Jumapili kuna watu walinifuata na kuniambia kuna mtoto anateswa na mlezi wake.

 

“Waliponiambia hivyo, nikawaambia hao walionifuata, twende nao kwa huyo mama tukamuone huyo mtoto.

“Tuliposogea nyumbani kwa mwanamke huyo, nikaona watu wengi hasa akina mama wamezingira nyumba yake.

 

“Hali ilikuwa mbaya kusema kweli, ikabidi nitumie busara kuwatuliza watu wenye hasira ambao walikuwa wakimzonga mwanamke huyo huku wengine wakimsukumasukuma.”

Aliongeza kwamba, alipoona watu wanazidi kumsonga Amina, ikabidi awasiliane na polisi ambapo walimchukua mtuhumiwa na kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi, Buza ambako mwanamke huyo alihojiwa.

 

“Polisi walipomhoji kuhusu tuhuma za kumtesa mtoto, alikiri kufanya hivyo na kuomba radhi kwamba hatorudia tena kosa kama hilo,” alisema Nyamrasa.

Inaelezwa kuwa, baada ya polisi kupima maelezo ya mwanamke huyo, walimpa onyo na kumruhusu arudi nyumbani na mtoto huyo wa ndugu yake akaendelee kumlea.

 

JIRANI WAFUNGUKA

Mmoja kati ya wapangaji wenzake na Amina, alimwambia mwandishi wetu kuwa, mwanamke huyo amekuwa na tabia ya kumtesa mtoto huyo kwa kumfanyisha kazi nzito na kumpiga.

 

“Yaani mtoto amekuwa akiamshwa usikuusiku na kurundikiwa vyombo vya kuosha na kazi nyingine nyingi.

“Yaani mtoto atahangaika na kazi mchana kutwa, akikosa kidogo anapigwa mpaka huruma,” alisema mpangaji mwenzake na Amina kwa sharti la kutotajwa jina.

 

Mpangaji mwingine kwa sharti kama la mwenzake, alisema wao kama wazazi wameumizwa na tabia hiyo ndiyo maana wakaamua kuchukua hatua ya kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

“Mara kwa mara amekuwa akimpiga, na siyo kumpiga kidogo, anampiga mno na kumnyanyasa jambo ambalo ni baya kwa mtoto.”

AMINA AJITETEA

Kufuatia sakata hilo, mwandishi wetu alimtafuta mtuhumiwa ambaye alijitetea kwa kusema:

“Huyu mtoto ni wa mdogo wangu kabisa, amenikabidhi niishi naye, hivyo ni damu yangu.

 

“Siwezi kuitesa damu yangu, nimekuwa nikimchapa kwa lengo la kumfundisha; sikuwahi kuwa na kusudio la kumtesa.

“Kuna mambo kadhaa ninapomuelekeza yeye hataki kunielewa. Nilimzuia kula kwa watu lakini hanielewi.

 

“Nimemkataza tabia ya kukojoa kitandani nayo pia hanielewi, sawa ni mtoto lakini ana uwezo wa kuongea lolote, iweje mkojo ukimuuma haniamshi?

“Hivyo nikaona njia pekee ya kumrekebisha ni kumuadhibu, lakini baadaye ndipo majirani zangu wakakusanyana na kuanza kunifanyia vurumai,” alisema Amina.

Akizungumzia ishu ya kupelekwa polisi, mwanamke huyu alisema ni kweli alifikishwa polisi, akatubu makosa yake na kuruhusiwa kuendelea kuishi na mtoto wa ndugu yake kwa mapenzi yote.

“Mapaka sasa naishi naye vizuri tu hakuna ubaya wowote ambao namfanyia na maisha yanaendelea,” alisema Amina.

Leave a Comment