
MASUALA ya usajili kwenye soka hivi sasa yamebadilika sana. Wachezaji wamekuwa wakinunuliwa kwa fedha nyingi tofauti na zamani.
Tukirudi nyuma mwaka 1928, Arsenal ilimsajili David Jack kwa pauni 1,890, lakini kipindi hiki tumeshuhudia Neymar ametoka Barcelona na kwenda PSG kwa Zaidi ya pauni 190m.
Lakini katika suala la usajili, ishu ya kupatia au kukosea lazima liwepo. Kuna nyota licha ya kusajiliwa kwa fedha nyingi, lakini wanashindwa kuonesha makali yao katika timu mpya ingawa wapo wanaoweza kuwika.
Hapa kuna orodha ya nyota wa kizazi hiki ambao wamesajiliwa kwa zaidi ya euro 100m na walichokifanya kwenye timu zao mpya.
NEYMAR
Huu ulikuwa usajili wa aina yake kwani uliteka vyombo mbalimbali vya habari duniani kutokana na matajiri wa PSG walivyovunja kibubu kwa kutoa euro 222m na kumchukua kutokea Barcelona mwaka 2017.
Inaelezwa kuwa, Neymar aliondoka Barcelona ili kwenda kujijenga na kutengeneza utawala wake kwa kushinda mataji makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa PSG, hali itakayomfanya awe na makali zaidi ya kuibeba Brazil na kutwaa Kombe la Dunia.
Hayo yote hayajatimia ingawa alianza vizuri katika makazi yake mapya. Majeraha ndiyo yanatajwa kuwa chanzo cha kushindwa kufikia malengo huku ujio wa Kylian Mbappe kikosini hapo ukaharibu kila kitu. Hivi sasa anajipanga kurudi Barcelona.
KYLIAN MBAPPE
Msimu mmoja baada ya Neymar kutua PSG, Mbappe akawasili akitokea Monaco.
Alianza kucheza kwa mkopo, baadaye akasajiliwa kwa euro 135m, hivi sasa anahusishwa kwenda Real Madrid.
Kwa muda wake hadi sasa, Mbappe anazidi kuwa moto na anatabiriwa kufanya makubwa zaidi.
JOAO FELIX
Baada ya kuwa na msimu bora ndani ya Ureno akiwa na Benfica, msimu huu Joao alitua Atletico Madrid kwa euro 126m.
Akiwa na miaka 19, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga hat trickkwenye Europa League na alitwaa Tuzo ya Golden Boy. Wakati huo bado ni mchezaji wa Benfica.
Tangu atue Atletico, ameonekana kama amepotea kwani katika mechi 20 amefunga mabao manne.
PHILIPPE COUTINHO
Barcelona ni kama walipoteza euro zao 120m kwa kumsajili Coutinho kutoka Liverpool kwani alishindwa kufiti kwenye mfumo wa Kocha Ernesto Valverde, akatolewa kwa mkopo.
Kwa sasa yuko Bayern akicheza kwa mkopo lakini huko ameshindwa pia kuwashawishi waweze kumsajili.
Akiwa Barcelona alicheza mechi 76 na kufunga mabao 21, akatoa asisti 11.
ANTOINE GRIEZMANN
Baada ya miaka mitano kuwa chini ya Kocha Diego Simeone, msimu huu mwanzoni akatua Barcelona kwa euro 120m akitokea Atletico ambapo huko alicheza mechi 257 na kufunga mabao 133.
Griezmann ameanza kwa kiwango cha chini ndani ya Barcelona. Amecheza mechi 37 na kufunga mabao 14, huku akitoa asiti nne.
OUSMANE DEMBELE
Dembele alitajwa kuwa mrithi wa Neymar ndani ya Barcelona ambapo alitua mwaka 2017 kwa euro 105m.
Usajili huu umeshindwa kutamba kabisa kutokana na majeraha yanayomkabili Mfaransa huyu aliyetokea Dortmund. Tayari amekosa mechi 86 ndani ya msimu mitatu.
PAUL POGBA
Pogba alirudi Man United akitokea Juventus mwaka 2016 kwa kiasi cha euro 105m.
Ameichezea Man United michezo 150 na kufunga mabao 31, huku akitoa asisti 31. Msimu huu kidogo amekumbwa na changamoto ya majeraha ambayo inamtesa sana ingawa tayari amepona kwa sasa.
EDEN HAZARD
Msimu huu, Hazard amejiunga na Real Madrid akitokea Chelsea akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Lakini ameanza vibaya ndani ya Madrid ambao walimwaga zaidi ya euro 105m kumsajili. Majeraha ndiyo yanamtesa. Amecheza mechi 10 na kufunga bao moja.
CRISTIANO RONALDO
Ronaldo alitua Madrid mwaka 2009 na kufanya makubwa akitokea Man United. Hivi sasa anaitumikia Juventus ambako alitua kwa zaidi ya euro 100m.
Akiwa Madrid, alitwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akafunga mabao 450 katika mechi 438.
Kutua kwake Juventus ilionekana kama ndiyo mwisho wa safari, lakini kwenye mechi 75, amefunga mabao 53 na kutoa asisti 14.
GARETH BALE
Euro 100m ziliwatoka Madrid kwa kumchukua Bale kutokea Tottenham. Kiasi hicho cha fedha hawakutoa bure kwani ni mchezaji ambaye amecheza kwa mafanikio makubwa ndani ya klabu hiyo.
Bale amekuwa bora akiwa hapo na ameisaidia Madrid kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amefunga mabao 105 na kutoa asisti 65 katika mechi 249.
ARIS, Ufaransa