×

Morrison Ana Mkataba wa miaka Miwili Yanga

KLABU ya Yanga kupitia Kampuni ya GSM imemaliza utata sakata la kiungo wa timu hiyo, Bernard Morrison kwamba tayari ana mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.

 

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya kiungo huyo kusikika kwenye vyombo vya habari akieleza kwamba kwa sasa yupo njia panda kufuatia kula dola 5,000 kutoka Simba, ambayo alipewa na wakala wake na ndio maana hakusafiri na timu kwenda Shinyanga.

 

Akizungumza Dar es Salaam kwenye kituo kimoja cha radio, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM , Hersi Said alisema anachojua mchezaji huyo ni mali hali ya Yanga, kwani bado ana mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kuitumikia timu hiyo.

 

“Ninachofahamu ni mchezaji halali wa Yanga, mkataba wake wa awali wa miezi sita bado mwezi mmoja unaisha tarehe 14 Julai lakini kutokana ubora wake, tulimsainisha mkataba mpya wa miaka miwili, ambao utaanza Julai 15 na utaisha mwaka 2022,” alisema Said.

 

Alisema baada ya kusikia sauti ya mchezaji huyo ambaye kwa sasa hajulikani halipo, uongozi wa Yanga una njia sahihi ya kupelekea malalamiko kwenye idara husika na kuona jambo linashughulikiwa kwa haraka.

 

Said alisema kama kuna mtu au timu inamhitaji mchezaji huyo wanapaswa kupita njia sahihi, huku akieleza sababu ya Morissoni kushindwa kusafiri na kikosi hicho kwenda Shinyanga halihusiani na masuala ya mkataba.

 

Morrison alieleza kwamba wakala wake alipokea dola 10,000 kutoka kwa kiongozi wa Simba, ambaye anatamani ajiunge na kikosi hicho, ambapo nusu ya fedha hiyo alipewa mchezaji huyo na nyingine amechukua wakala ili kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi mkataba utakapomalizika.

Leave a Comment