×

Ummy: Waganga Wakuu Wasimamie Wagonjwa wa Sikoseli -Video

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, leo Juni 19, 2020 amewaagiza waganga wakuu wa mikoa wahakikishe wanasimamia huduma za wagonjwa wa Sikoseli zinatolewa katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo katika mikoa wanayoisimamia.

 

Ameyasema hayo katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake ambako amewasisitiza waganga kuanzisha kliniki maalum za Sikoseli katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya.

 

Taarifa hiyo imesema kwamba ugonjwa huo husababishwa na  wahusika kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili, yaani baba na mama ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 15-20 ya Watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya  ugonjwa huo.

Taarifa kamili iliyotolewa na ofisi hiyo ni ifuatayo chini:

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU SIKU YA SIKOSELI DUNIANI
TAREHE 19 JUNI, 2020
Ndugu Wananchi,
Kila ifikapo tarehe 19 Juni ya kila mwaka Tanzania hujumuika na nchi nyingine Duniani katika kuadhimisha siku ya Sikoseli. Lengo la Maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Sikoseli ili kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huu. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2020 ni: “Huduma bora ya Sikoseli kwa kila mhitaji’ Sambamba na kauli mbiu hiyo, tunao ujumbe mahsusi katika kuadhimisha siku hii ambao ni: “Chukua hatua panua uwigo” Kauli mbiu hii pamoja na ujumbe mahususi unalenga kuwashirikisha wadau katika utoaji wa huduma za Sikoseli katika vituo vyote ya Tiba ili kumfikia kila mtanzania mwenye kuhitaji.

Ndugu Wananchi,
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto 1000 duniani huzaliwa na Sikoseli kila siku. Pia, Takwimu zinaonyesha kuwa, watoto takribani elfu kumi na moja (11,000) huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila mwaka hapa nchini, hii ni sawa na watoto 8 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa.

 

Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Sikoseli, nchi inayoongoza duniani kwa ugonjwa wa sikoseli ni Nigeria ambapo katika nchi hiyo watoto 20 – 30 kati ya 1000 huzaliwa na tatizo la Sikoseli. Nchi inayofuata ni India ambayo kwa mujibu wa takwimu inaonyesha kuwa, watoto 14 kati ya 1000 huzaliwa na tatizo la sikoseli, na nchi ya tatu ni DRC Kongo ambapo watoto 13 kati ya 1000 huzaliwa na sikoseli kila mwaka. Kwa sasa, Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye Sikoseli. Takribani watoto 7 kati ya watoto 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki nchini kutokana na Sikoseli.

 

Ndugu Wananchi,
Ugonjwa wa Sikoseli husababishwa na kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 15-20 ya watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya Sikoseli.

 

Ndugu Wananchi,
Ili kuhakikisha tunapunguza madhara na vifo kwa watoto wanaozaliwa na Sikoseli, Serikali imechukua hatua muhimu zifuatazo:-
Kujumuisha Sikoseli katika Mpango Mkakati wa Taifa wa pili wa magonjwa yasiyoambukizwa (2016-2020).
Kuanzisha kikosi kazi cha Taifa cha Sikoseli (2017)
Kuzindua Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa unaojumisha Sikoseli mwezi Novemba 2019.

 

Ndugu Wananchi,
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na hatua hizi muhimu zilizobainisha hapo juu ni haya yafuatayo:-
Ongezeko la Wagonjwa wa Sikoseli wanaotibiwa katika vituo vya tiba kutoka 32,457 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 61,212 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 88.6.
Huduma za maabara na utambuzi wa ugonjwa wa Sikoseli zimeboreshwa:
Mwaka 2015 ni Hospitali ya Muhimbili pekee iliyokuwa na uwezo wa kuthibitisha ugonjwa wa Sikoseli kwa kutumia ‘HB Eletrophoresis’. Kwa mwaka 2020 kipimo hiki kinafanywa na Hospitali 6 zikijumuisha Hospitali za Bugando, Mbeya, Hospitali za binafsi-St Gemma, Aga Khan na Regency.
Hivi karibuni tunatarajia kuanza kutoa huduma za vipimo vya papo kwa hapo (Rapid Diagnostic Tests) katika Hospitali zote za Mikoa, Wilaya na Vituo vya Afya

 

Dawa muhimu zinazotumika kutibu ugonjwa wa Sikoseli zimeingizwa katika mwongozo wa Tiba wa Taifa (Standard Treatment Guideline).

Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma ya upandikizaji wa uloto (bone marrow transplant) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Uwepo wa kitabu maalum kidogo (pasipoti) kwa wagonjwa wa Sikoseli kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa hao.

Tumeendelea kutoa elimu ya kupunguza visa vya sikoseli kwa vijana kwa kuzingatia kupima kabla ya kuingia kwenye mahusiano
Kuendelea kufanya tafiti za Sikoseli nchini zitakazotusaidia kufanya maamuzi ya Kisera yenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi.
Kukamilika kwa Mwongozo wa utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wa Sikoseli ambao nitauzindua leo.

 

Ndugu Wananchi,
Mafanikio niliyoyaeleza hapo juu yanatokana na uboreshwaji wa huduma za Afya katika ngazi mbalimbali. Hata hivyo, Ili kuendelea na upatikanaji wa huduma za afya na hususan katika eneo la ugonjwa huu wa sikoseli ninaelekeza yafuatayo:-

Waganga Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanasimamia huduma za Wagonjwa wa Sikoseli zinatolewa katika Hospitali na vituo vya Afya vilivyopo katika Mikoa wanayoisimamia. Aidha, wanatakiwa kuanzisha kliniki maalum za Sikoseli katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutoa elimu ya afya mashuleni, vyuoni na jamii kwa ujumla kuhusiana na tatizo la Sikoseli.
Kwa watendaji wa wizara wahakikishe wanasambaza Mwongozo wa ugonjwa wa sikoseli ambao unazinduliwa leo katika mikoa yote ili kuhakikisha mipango mizuri iliyomo katika Mwongozo huu inatekelezwa.

 

Mwisho,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitumie fursa hii kuwashukuru wadau wa Maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sikoseli. Kipekee napenda kuwashukuru NOVARTIS FOUNDATION kwa kutoa ufadhili wa kuchapisha Mwongozo wa Sikoseli kama sehemu ya maadhimisho ya mwaka huu.

Vile vile, natoa wito kwa wadau wa maendeleo katika sekta ya afya kuendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada mbalimbali ili kuhakikisha tunapunguza tatizo hili. Wizara ya Afya inawashukuru wadau wote wa ndani nan je ya nchi wanaotuunga mkono.

Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kuzindua Mwongozo wa Kitaifa wa Matibabu ya Sikoseli.

Imetolewa na:

Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO

Leave a Comment