×

Kenyatta Akwepa Uwezekano Kenya Kuwa na Waziri Mkuu

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amekataa kufutilia mbali uwezekano kwamba wadhifa wa waziri mkuu huenda ukabuniwa katika kura ya maoni ijayo kama njia ya kumfanya kuwa na madaraka hata baada ya muda wake wa kikatiba wa mihula miwili kama rais kukamilika.

 

Kenyatta anaachilia madaraka 2022. Katika mahojiano na gazeti la Financial Times,  Uhuru alikataa kuzungumzia kuhusu ‘nyadhfa za kisiasa ambazo hazipo’.

 

Hata hivyo, alisema waziwazi kwamba hatosalia kuwa rais baada ya kukamilika kwa mihula yake miwili, akisema kwamba katiba na watu wa Kenya wako wazi kuhusu suala hilo.

 

”Wakenya wanaelewa kuhusu mihula miwili ya urais tangu 2002, wakati ilipoanza kutekelezwa . Hakuna rais hata mmoja aliyevunja sheria hiyo . Na sina nia kuwa rais wa kwanza kufanya hivyo’,’ alisema.

 

Amesema kwamba Kenya itaandaa kura ya maoni hivi karibuni, kulingana na yeye ili kubadilisha baadhi ya vifungu vya katiba ukweli ambao pia walioitengeneza wanakubaliana nao.

 

Pia alizungumzia wasiwasi kuhusu biashara huru inayojadiliwa kati ya Kenya na Marekani, akisema yatakuwa majadiliano ya usawa licha ya tofauti ya kiuchumi na kisiasa ya mataifa hayo mawili.

 

Mashirika mengi ya wanaharakati  ambayo yanadai kwamba makubaliano hayo ya kibiashara yatakuwa mabaya kwa uchumi wa Kenya, yalituma ujumbe wa kupinga chini ya alama ya reli #NoToKenyaUSFTA.

 

Pia alikuwa na ujumbe kwa wale wanaoshiriki katika maandamano ya Black Lives Matter nchini Marekani na duniani kwa jumla : All Lives Matter, “lakini hakufai kuwa na ukandamizaji wa kundi lolote katika jamii.”

 

Tangu naibu wa rais William Ruto kuanza kampeni za mapema kugombea urais 2022, changamoto kuu ya  Kenyatta imekuwa iwapo atamaliza muhula wake wa pili kama kiongozi ambaye alifeli kutimiza ahadi zake kwa Wakenya.

Ili Kutekeleza ajenda yake ya masuala manne makuu serikalini, alimtangaza Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiangi kama mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji wa maendeleo na mawasiliano katika baraza la mawaziri, hatua inayomzuia naibu wa rais katika kukagua miradi ya serikali.

Lakini la kushangaza ni kwamba uteuzi huo ulimpatia Matiangi uwezo mkubwa wa kusimamia miradi yote ya serikali.

Kwa miezi kadhaa , naibu huyo hajakuwa akihudhuria hafla za rais katika Ikulu ya rais na pia amekosa kushirikishwa katika mikutano ya baraza kuu la usalama ambapo yeye ni mwanachama.

Wakati mmoja naibu huyo wa rais alisikika akisema kwamba kuna njama ya kumzuia kumrithi rais Uhuru Kenyatta na ‘mfumo’.

Naibu huyo alinukuliwa mnamo mwezi Machi mwaka huu ,akisema kwamba mfumo huo bila kutoa ushahidi ulikuwa unapanga njama dhidi yake.

”Wale walio katika mfumo huo wanajigamba kwamba sitakuwepo hivi karibuni”, naibu huyo aliandika katika mtandao wake wa Twitter.

”Na kwasababu mfumo huo hauwezi kumchagua mtu yeyote, unaweza kuua. lakini kuna Mungu aliye juu mbinguni”, alimaliza.

Leave a Comment