
RAIS John Magufuli amesema huwa anasikitishwa kuona watu ambao amewapa nafasi na kuwaamini wanashindwa kutekeleza yale ambayo amewatuma kwenda kufanya na badala yake wanakwenda kufanya ya kwao huku akitumia nafasi hiyo kuzungumzia vijana ambao amewapa nafasi lakini hawaridhiki nazo.
Alikuwa akizungumza leo Juni 22, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kumwapisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta, na baadaye akashuhudia wakuu wa mikoa ya Arusha na Morogoro wakiwaapisha wakuu wa wilaya za Arusha, Monduli na Morogoro.
Wengine walioapishwa na wakuu hao wa mikoa ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima na Mkurugenzi wa Kaliua, Jerry Pima.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi waliokuwa kwenye nafasi kutekeleza majukumu yao kwa kuheshimu sheria na viapo walivyoapa kikiwemo kiapo cha maadili ya viongozi wa umma.

“Niliwaapisha leo nendeni mkazingatie viapo vyenu, mmeapa viapo vya maadili nendeni mkazingatie. Huwa nasikitika ninapoona watu ambao umewateua na kuwaapisha lakini wakienda maeneo yao ya kazi hawafanyi kazi viapo vyao.
“Mkoa wa Arusha katika kipindi cha miaka miwili Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji Arusha walikuwa hawalewani, wao ni kugombana tu. Walikuwa wanafanya kazi lakini waliniudhi kwa kutoshirikiana. Sasa nimewateua ninyi sitaki yakatokee hayo. Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kafanyeni kazi zenu vizuri, “amesema .
Hata hivyo Rais Magufuli amesema kuwa tatizo la vijana ukiwapa nafasi wanashindwa kuridhika na hizo nafasi, wanasahau miaka bado ni mingi sana.
“Kwa sababu Takukuru na IGP mpo hapa nendeni mkawaonye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha pamoja na Mkuu wa Takukuru Arusha.
“Ilikuwa niwatoe ila nimewasamehe, lakini sijawasamehe moja kwa moja wakifanya makosa nawaondoa. Wafanye kazi ambazo nimewatuma na badala ya kwenda kufanya kazi zao. Mnafahamu kazi ambazo walikuwa wanazifanya katika kipindi hiki kifupi, nendeni mkaawambie wafanye kazi nilizowatuma, wasimamie maadili, wasimamie sheria,”amesema Magufuli.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwenda kutatua migogoro ya ardhi iliyopo katika baadhi ya wilaya katika mkoa huo. Kulikuwa kuna mgogoro wa Kanisa na Shule ambapo kulikuwa na maamuzi kwamba litafutwe eneo lingine na Jiji lilipe Sh.milioni 400 .
“Nilishatoa maamuzi wakitaka kuongeza shule wajenge ghorofa lakini sio kwenda kutafuta eneo jingine,” alisema.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba kuna eneo la wazi ambalo kwa muda mrefu viongozi wa dini ya Kiislamu wamekuwa wakiiomba eneo hilo lakini msimamo wa viongozi wote waliopita kuanzia awamu ya pili mpaka awamu ya nne wametoa maelekezo eneo hilo kubaki kama lilivyo lakini sasa limeibuka tena.
“Open space (eneo la wazi) inabaki kuwa open space, mgogoro ulianza enzi ya Mzee Mwinyi akakataa, Mzee Mkapa akakataa, Mzee Jakaya Kikwete kakataa, na sasa limeletwa tena kwangu. Msimamo ni uleule ambao uliwekwa na viongozi waliotangulia.
“Ila ikitokea shughuli kwa mfano Maulid au ibada nyingine yoyote ya kidini eneo hilo litumike bure. Tatizo limeletwa na Mkuu wa Mkoa ili aonekane mzuri. Hivyo wewe Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi msiingie kwenye tatizo hilo,”amesema Magufuli.
Amezungumzia pia ujenzi wa stendi ya mabasi ya Mkoa wa Arusha ambapo amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kuhakikisha anakwenda kufanikisha ujenzi huo.
“Mkasimamie hilo, wanannchi wa Arusha wamecheleweshwa kupata stendi. Viongozi waliopita wamekuwa wakibishana sasa wakabishanie huko mtaani. Kama kugombana na kubishana kabishane na mkeo na mtoto wako. Ni matumani yangu ninyi ambao nimewateua mtakwenda kufanya yale ambayo tunayatarajia. Arusha tumepeleka miradi mingi mno na wana-Arusha wanafahamu,”amesema rais.