×

Vanessa Aibua Vilio Kuacha Muziki

NI kama msiba! Ndicho kilichotokea baada ya mwanamuziki mkubwa wa Afro-Pop kutoka Tanzania na Afrika, Vanessa Mdee ‘V-Money’ kutangaza rasmi kuacha muziki ambapo ameibua vilio kama vyote.

 

Vanessa amesema ameamua kufanya hivyo kwa roho moja kutokana na matendo yaliyomo ndani ya tasnia ya muziki.Akizungumza kwenye kipindi chake cha redio mtandaoni (podcast) Vanessa amesema tasnia ya muziki imejaa mambo ya ajabu yasiyoaminika machoni pa watu.

 

“Kilichonifanya nichukue likizo kwenye muziki ilikuwa ni kuchagua maisha yangu na muziki.“Unajua unapoingia kwenye tasnia ya muziki, watu wanakuambia upande mmoja tu wa mazuri na kusahau mabaya.

“Kiukweli tasnia ya muziki imejaa mabaya mengi na ilibidi nichague kuendelea kwenye ubaya au maisha yangu,” amesema Vanessa na kuongeza;“Kwa wale wasanii Waafrika ambao wanatamani kuishi the American dream au wafike Marekani ndipo wafanikiwe huko, waache hizo ndoto, kwa sababu ni kugumu mno.“Akina Selena Gomez (mwanamuziki mkubwa duniani) huku wako wengi na hawana nafasi.“Kama unataka kung’aa, ng’ara huko uliko, ng’ara nyumbani.

 

”Matamshi ya Vanessa yamesababisha mamilioni ya mashabiki na wafuasi wake zaidi ya milioni 6 pale Instagram kuangua vilio wakiamini sasa wanakwenda kukosa vitamin kutoka kwenye muziki mtamu wa Vanessa.“Inahuzunisha sana, nampenda Vanessa na ninapenda muziki wake,” ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya mwanadada huyo kuacha muziki.

 

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi hao walikuwa na mtazamo tofauti;“Asante Mungu kwa kumnusuru mwanao. Na asante Vee kwa kusema ukweli, utawasaidia vijana wengi sana waliodhani muziki ndiyo maisha, maana kwa kweli kwa muziki wa Tanzania kwa wanawake, wewe ulikuwa ni nembo.

 

“Kusema kweli kutafumbua wengi sana. Big up kwa mama yako, kuona kuwa hakuna cha thamani kama roho yako. Ulimwengu huu kila kitu kinapita, cha msingi ni kuwa na amani na Mungu ndani yako.”Ikumbukwe kuwa kwa sasa Vanessa anaishi Atlanta nchini Marekani na mwenzi wake, Rotimi ambaye ni mwigizaji na pia ni mwanamuziki.

STORI: KHADIJA BAKARI, DAR

Leave a Comment