
VIONGOZI wa Mkoa wa Arusha waliosamehewa na Rais John Magufuli wakati alipotengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji hilo wamehamishwa vituo vya kazi.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo, Frida Wikes amehamishiwa Makao Makuu na Kamanda wa Polisi Mkoa, Jonathan Shanna, amehamishiwa katika Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, inaelezwa kuwa mwingine aliyeathirika na uhamishwaji huo ambao unaelezwa kuwa na lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ni Mkuu wa Usalama Mkoa wa Arusha.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kuwasamehe Kamanda Shanna na Mkuu wa Takukuru Arusha kutokana na kufanya kazi tofauti na alizowatuma, ingawa aliweka wazi kuwa hajawasamehe moja kwa moja.