×

Kapombe aivuruga Simba SC

”UONGOZI wa Klabu ya Simba umekiri kuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kushindwa kujua ukubwa wa jeraha alilolipata nyota wao, Shomari Kapombe baada ya kukanyagwa na kiungo wa Azam FC, Frank Domayo.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema kuwa uchunguzi zaidi juu ya ukubwa wa jeraha la Kapombe aliyeumia juzi Jumatano katika mchezo wa Kombe la FA, unafanyika baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
“Mpaka sasa hatujajua kuhusu ukubwa wa jeraha la Kapombe kwa kuwa uchunguzi wa kina utafanyika leo (jana) baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa awali, nadhani kwa sasa tuendelee kusubiri ripoti ya madaktari kuhusu ukubwa wa jeraha alilolipata ili kujua ni kwa namna gani tumeathirika kutokana na tukio lile” alisema Rweyemamu.
Upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alieleza kuwa kuna wasiwasi wa kumkosa Kapombe kwenye mechi zilizosalia, lakini naye anasubiri majibu ya vipimo.
“TFF walimpa adhabu Mkude ya kutocheza mechi mbili, kwa hiyo nafikiri kwa tukio la leo (juzi) ni baya, TFF pia wanatakiwa wachukue hatua stahiki,” alisema Sven.Daktari wa Simba, Yasin Gembe alipoulizwa alisema: “Muda huu (jana mchana) tuko hospitali kwa ajili ya vipimo siwezi kutoa tamko kabla ya majibu yake.”

Leave a Comment