


WANACHAMA wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wametakiwa kufika kwenye ofisi za Mfuko huo zilizoenea katika mikoa yote nchini ili kuhakiki taarifa zao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya 44 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye banda namba 13 la Mfuko huo kwenye viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Meneja wa PSSSF mkoa wa Temeke, James Mlowe alisema mwanachama akifika kwenye ofisi yoyote ya PSSSF utaratibu na mahitaji yako vile vile hivyo amewahimiza kufanya hivyo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na kutohakiki taarifa.
Lakini pia amewaalika wanachama watakaotembelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere kwenye maonesho hayo ya biashara maarufu kama sabasaba, wataweza kujipatia huduma zote kama zinavyotolewa kwenye ofisi za Mfuko kwenye mikoa yote nchini.
“Tulichofanya mwaka huu tumehamisha miundombinu na vifaa vyote vya kutoa huduma vinavyopatikana kwenye ofisi zetu ikiwemo makao makuu, hivyo mwanachama anapofika kwenye banda letu anapata huduma zote ikiwemo, taarifa za michango, mafao, pensheni na mafao yanayotolewa na Mfuko” alifafanua Bw. Mlowe.