
MOROGORO: Unamkumbuka yule pedeshee Dallas wa Wolper? Basi kama ni hivyo tuukubali ule usemi kwamba ‘true love never dies’! Hicho ndicho kimejiri kwa wachumba zilipendwa; staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper na mfanyabiashara Ramadhan Mtoro ‘Dallas’ ambapo mwanadada huyo anakiri kuwa, huwa anamnunulia jamaa huyo kanzu na kofia.
Kwa upande wake Dallas, anasema kuwa, hata akifa sasa hivi, mwanamke ambaye anampenda ni staa huyo.
Dallas anasema endapo atapata pesa kama zamani, basi lazima amuoe Wolper.Katika mahojiano maalum na Gazeti la IJUMAA mkoani Morogoro akiwa kwenye mazishi ya mke wa meneja wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Hamis Taletale ‘Babu Tale’, Dallas alisema watu wengi hawajui, lakini ukweli ni kwamba, anampenda Wolper.

Dallas anasema hajaona mwanamke mwingine wa kumpenda kwenye maisha yake yote yaliyobaki duniani zaidi ya Wolper.“Huyu ndiye mwanamke wa maisha yangu. Hilo litaendelea kuishi kwenye maisha yangu hadi mwisho wa uhai wangu.“Ninampenda sana Wolper na nitaendelea kumpenda siku zote,” anasema Dallas ambaye baada
ya uchumba wake na Wolper kuvunjika, alioa mwanamke mwingine na bado yupo naye.Aliongeza kuwa, ikitokea akapata pesa tena kama kipindi kile, basi mtu ambaye atamuoa tena kwa harusi kubwa ni Wolper.
“Nakwambia mimi nikibahatika kupata pesa kama kipindi kile, kazi yangu itakuwa ni moja tu, kumuoa Wolper, sijaona mwanamke mwingine kwenye maisha yangu.” anasema Dallas huku akiinua mikono juu kumuomba Mungu amsikilize dua yake.
Wakati Dallas anasema hayo mbele ya Wolper, mwanadada huyo yeye alimpokelea mazungumzo ambapo alisema, watu wanadhani wana ugomvi, lakini ukweli ni kwamba ni marafiki wa karibu mno na wanapendana, ndiyo maana huwa anamnunulia kanzu na kofia.
“Sina tatizo kabisa na Dallas na tunapendana mno, tunapiga stori na akiwa na kitu chochote lazima anakuja pale dukani kwangu (Sinza-Makaburini, Dar) tunaongea.
“Hata kanzu na kofia huwa ninamnunulia mimi, sisi siyo maadui, ni marafiki wakubwa sana,” anasema Wolper ambaye naye alikuwepo kwenye mazishi hayo.Wolper na Dallas walivuma mwaka 2012 baada ya jamaa huyo kuwa na pesa chafu, kiasi cha kufanya kufuru mbalimbali ikiwemo kumuonga staa huyo gari aina ya BMW X6 kabla ya uchumba wao kuota mbawa.
Stori: Imelda Mtema, Ijumaa