
KUNA ule usemi usemao kwamba, unaweza kulala maskini kisha ukiamka tajiri!
Ndivyo ilivyo kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva anayechipukia: Maneno Issa ‘Man Mo’. Huyu mwamba ni almasi iliyoibuliwa na Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ baada ya kueleza waziwazi hisia zake kwa mwanamuziki huyu kupitia wimbo wake unaotamba kwa sasa wa Sweet Kitunguu.
JPM alifunguka hayo alipokuwa kwenye ziara ya kikazi pale wilayani Kisarawe, Pwani.
Man Mo anasema kuwa, hakutegemea mtu mkubwa kama Rais Magufuli kusikiliza nyimbo zake, lakini pamoja na hayo, alipita kwenye msoto wa hatari hadi Magufuli alipoamua kuweka wazi anasikiliza nyimbo zake na ni kijana mwenye kipaji kikubwa.
Man Mo amefanya mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, ambapo anafunguka namna alivyopokea taarifa hizo za kukubalika hadi na JPM;
IJUMAA WIKIENDA: Mambo vipi na hongera kwa kazi nzuri kiasi cha kutajwa na Rais, siyo jambo dogo…
MAN MO: Asante sana. Ni kweli siyo kitu kidogo kabisa, ninamshukuru mno Mwenyezi Mungu kwa hilo.
IJUMAA WIKIENDA: Siku ambayo Rais Magufuli alikutaja kwenye mkutano wake na wananchi wa Kisarawe kuwa anasikiliza sana wimbo wako wa Sweet Kitunguu, ulisikia mwenyewe au ulipewa taarifa na mtu?
MAN MO: Sikusikia mwenyewe, nilipewa taarifa na watu. Hata mtu wa kwanza kuniambia, niliona ananidanganya tu au amezoea kunitania, lakini nikaanza kupokea simu mfululizo na wengine wakinitumia video ya Mheshimiwa Rais akinitaja, ndipo nikaamini.
IJUMAA WIKIENDA: Ulijisikiaje siku hiyo?
MAN MO: Kwa kweli siwezi hata kuelezea, yaani nilijiona wa tofauti kabisa, siku ile sikulala kabisa, kifupi nilichanganyikiwa.
IJUMAA WIKIENDA: Baada ya kukubalika hadi kwa Rais Magufuli, vipi wasanii wenzako wanakuchukuliaje?
MAN MO: Huwezi kuamini, ninapokea simu nyingi sana kutoka kwa wadau mbalimbali wa muziki Bongo na hata kufanya mahojiano kwenye media tofautitofauti. Zamani haikuwa hivyo kabisa.
IJUMAA WIKIENDA: Wimbo wa Sweet Kitunguu umetengenezwa studio gani na kwa nini hauna video, badala yake ni vikatuni tu?
MAN MO: Sweet Kitunguu umetengenezwa Classic Sound chini ya Producer Mona Gangster. Kuhusu video, nilitaka kuweka utofauti na huwezi kuamini, watu wengi wameipenda sana aidia ya vikatuni.
IJUMAA WIKIENDA: Hadi sasa una nyimbo ngapi?
MAN MO: Nina nyimbo tatu tangu niingie kwenye gemu na hapa nipo studio kupika zawadi ya Rais wangu Magufuli. Natumia ala ileile ya Sweet Kitunguu, lakini maneno ni ya kumzungumzia yeye.
IJUMAA WIKIENDA: Baada ya Rais Magufuli kukutaja, umepigiwa simu za kazi?
MAN MO: Simu ni nyingi mno. Kama Instagram napokea meseji nyingi sana. Kwa kweli Mwenyezi Mungu amenifanyia makuu sana.
IJUMAA WIKIENDA: Mbali na Sweet Kitunguu, nyimbo zako nyingine ni zipi?
MAN MO: Kuna Hamida, Kuku Sekela na hii ya Sweet Kitunguu.
IJUMAA WIKIENDA: Kuna msoto wowote uliopitia kwenye muziki wako?
MAN MO: Sana tu mpaka nilishakata tamaa, maana nilijiingiza mpaka kuimba nyimbo za Injili ambapo niliimba Nyimbo za Jicho Langu na Nimuimbie, jambo ambalo lilisababisha nitengwe na familia yangu, lakini sasa hivi tuko sawa kwa sababu nimerudi kwenye dini yangu.
IJUMAA WIKIENDA: Wimbo wa Sweet Kitunguu umetunga mwenyewe au kuna mtu aliitunga na wewe ukaiimba?
MAN MO: Mimi ni mtunzi mzuri pia. Hata ule Wimbo wa Simama wa Lady Jaydee, nimemtungia mimi na wasanii wengi tu ninawatungia, hivyo nipo vizuri.
MAKALA: IMELDA MTEMA, BONGO