×

Mwanza: Polisi Yazima Tukio la Ujambazi Benki ya CRDB

TUKIO hili limetokea usiku wa Julai 07, 2020, majira ya saa 8.00 za usiku katika Benki ya CRDB, Tawi la Igoma, wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, baada ya kundi la majambazi kuvunja kwa nyuma eneo la jengo la benki hiyo ambayo imepakana kwa karibu na majengo mengine na kufanikiwa kukata bati la paa na dari (ceiling board) na kupata mwanya wa kuingia ndani ya benki hiyo.

 

Askari Polisi waliokuwa lindo katika eneo hilo walibaini kuwepo kwa mazingira yasiyo ya kawaida, walipozungukia jengo hilo kuchunguza kwa kina walibaini kuwepo kwa mmoja wa majambazi aliyekuwa tayari ndani akijaribu kutoka kupitia sehemu waliyovunja wakati wakiingia.

 

Askari walimwamuru ajisalimishe lakini alikaidi amri hiyo halali na walimrushia risasi iliyomjeruhi mkono na bega la kulia akalazimika kurudi ndani ya benki  na akakamatwa huku akiwa katika hali mbaya.

 

Mtuhumiwa alikimbizwa hospitali ya mkoa ya Sekou Toure kwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia akiwa bado njiani, mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kusubiri uchunguzi wa daktari na utambuzi.

 

Uchunguzi wa awali uliofanyika eneo la tukio kwa kushirikiana na meneja wa benki hiyo umebaini kuwa licha ya wahalifu hao kuingia ndani ya benki na kuvuruga droo za ofisi hizo lakini hawakuweza kufanikiwa kuiba fedha zilizokuwa zimehifadhiwa sehemu maalum.

 

Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji mkali wa kuhakikisha watuhumiwa wengine walioshiriki kupanga na kujaribu kutenda tukio hili wanakamatwa.

 

Leave a Comment