
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa amepanga kuutumia mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa leo kama kipimo kizuri kuelekea mchezo wa nusu fainali ya FA dhidi ya Yanga utakaopigwa Julai 12, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumatano, Sven alisema Namungo ni timu bora, hivyo anafurahia kupata kipimo hicho kabla ya kuwavaa Yanga kwa mara ya tatu msimu huu.

“Natarajia kutumia mchezo wetu dhidi ya Namungo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Jumapili ya Julai 12.
“Kila mtu anajua kuwa Namungo ni miongoni mwa timu bora, hivyo natarajia tutakuwa na mchezo mgumu na licha ya kwamba tayari tumetangaza ubingwa lakini tutapambana kusaka ushindi kwenye mchezo huo,” alisema Sven.
Kwenye mchezo huo dhidi ya Namungo, Simba inatarajiwa kukabidhiwa rasmi kombe lake la Ligi Kuu Bara ililolitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.
Na Joel Thomas, Dar es Salaam | Championi Jumatano, Julai 8, 2020