×

Anunua Barakoa ya Dhahabu Kujikinga na Corona

MWANAUME mmoja nchini India ametumia Sh milioni 8.6 kununua barakoa ya dhahabu ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Barakoa hiyo yenye uzito wa gramu 60, iliwachukua wasanifu wa bidhaa hiyo siku nane kumtengenezea mfanyabiashara Shankar Kurhade, barakoa hiyo maalumu.

“Ni nyembamba na ina mashimo madogo madogo yanayokuwezesha kupumua, sina uhakika iwapo itanilinda dhidi ya virusi, lakini nachukua tahadhari nyingine,” alisema Shankar.

Anapoondoka kwake kuelekea kwenye shughuli za kila siku, mfanyabiashara huyo hupenda kujistiri kwa dhahabu ikiwemo mshipi wake, shanga na mkufu vyote vyenye uzito wa takriban kilo moja.

Kurhade alisema alipata wazo la kutengenezewa barakoa ya dhahabu baada ya kuona katika vyombo vya habari mwanaume mmoja akivalia iliyotengenezwa kwa fedha.

“Kutokana na upekee wa hii barakoa yangu, nimekuwa nikipata usumbufu kutoka kwa watu ambao wanataka nipige nao selfie,” alisema.

Tangu kuibuka kwa maambukizi ya Virusi ya Corona duniani Desemba mwaka jana na kuanza kusambaa sehemu mbalimbali duniani, Nchi ya India imefanya uvaaji wa barakoa kuwa jambo la lazima katika maeneo ya umma.

Hadi kufikia Julai 6, mwaka huu, nchi hiyo ilikuwa na idadi ya watu 700,000 walioambukizwa Corona huku watu 19,707 wakipoteza maisha kutokana na virusi hivyo ambavyo vimechukua uhai wa watu 540,000 duniani.

MWANDISHI WETU, Risasi

Leave a Comment