
BAADA ya Simba jana kutoka 0-0 na Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, ilikabidhiwa kombe kutokana na kuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu huu.Baada ya kukabidhiwa kombe hilo, wakawa wanatamba wakiwaambia Yanga kwamba: “Hamtuwezi, tukikutana Jumapili tunawachapa na msimu ujao katika ligi tunakuwa tena mabingwa.
”Mchezo huo wa jana Simba ilikuwa inahitaji heshima kwa kuwa imeshamaliza kazi ya kutwaa ubingwa, huku Namungo FC ikihitaji kuongeza mbio za kubaki ndani ya tano bora.

Simba iliyokuwa ikimtumia mshambuliaji wake namba moja Meddie Kagere mwenye mabao 19, alishindwa kufurukuta mbele ya mikono ya Nurdin Barola ambaye alikaa imara kwenye lango lake.
Kipa wa Simba, Beno Kakolanya alianza jana ikiwa ni mchezo wake wa nane ndani ya Ligi Kuu Bara chini ya Sven Vandenbroeck alifanikiwa kuokoa hatari za Bigirimana Blaise ambaye alitolewa kwa ulazima dakika ya 40 baada ya kupata majeraha.

Matokeo hayo ya jana yameifanya Simba kufikisha pointi 81, imebakiwa na mechi nne za kukamilisha msimu huu.Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa Simba kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kutokana na kufanya hivyo, hivi karibuni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo alisema wataipa Simba kombe hilo jumlajumla.

Kumbuka Jumapili itacheza dhidi ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Timu hizo msimu huu zimekutana mara mbili katika ligi na Simba wameshindwa kutamba mbele ya Yanga, wamefungwa moja na sare moja.

SHEREHE ZA UBINGWA
Hamis Kigwangala, Waziri wa Maliasili na Utalii, ndiye aliyekabidhi taji la ubingwa huo kwa Nahodha wa Simba, John Bocco baada ya mchezo kumalizika.Baada ya kukabidhiwa kombe, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema ni mwanzo mzuri wa kutwaa mataji kwani wanataka kufikisha kumi mfululizo.

KURUDI DAR MAPEMA LEO
Leo Alhamisi, mabingwa hao wanatarajia kurudi Dar mapema saa 2 asubuhi, kisha wataanza kulitembeza kombe lao. Baada ya sherehe kumalizika, wataanza kuiwinda Yanga.Manara amesema: “Kuhusu mchezo wetu dhidi ya Yanga hatuna hesabu nao kwa sasa, tukimaliza kushangilia ubingwa ndiyo maandalizi yataanza.