×

Mti wa Tambiko Wazua Tafrani

IMANI za kimila zimezua jambo hasa baada ya mti unaodaiwa ni wa tambiko kukatwa na kuleta tafrani kwa wakazi wa Kata ya Mvumi Mukulu, mkoani Dodoma.

 

Mbali na sintofahamu kujitokeza kwenye jamii, malumbano makali yaliibuka kati ya Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Happiness Pesa na Chifu wa Kabila la Wagogo, Chifu Henry Mazengo wa Pili.

 

Chifu huyo amedai kwamba kitendo cha kukatwa kwa mti huo kwa ruhusa ya mtendaji, kimemuondolea mizimu yake aliyokuwa anaitumia kwenye kazi yake kimila.

Kwa msingi huo, chifu alimtaka aliyehusika kuukata mti huo kuwajibika kwa kumrejeshea mizimu yake.

 

“Mimi ninachotaka ni mizimu irudi kwa sababu hapa nilipo siwezi kufanya shughuli zozote za kichifu kwa sababu ‘watu’ wangu hawapo,” alisema chifu huyo.

Aliongeza kuwa, binafsi hawezi kuiita mizimu yake kwa sababu nyumba iliyokuwa inaishi, imeharibiwa.

 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji, Pesa alipohojiwa na mwandishi wetu kuhusu kuwajibika kwa kuharibu mizimu ya chifu, alisema yeye alikuwa hajui kwamba mti huo ulikuwa unatumika kwa shughuli za kimila.

Alisema kutojua huko, ndiko kulikomfanya atoe kibali kwa mwananchi mmoja katani hapo aukate kwa ajili ya matumizi yake binafsi.

 

“Kuna mwananchi aitwaye Joseph Paul alikuja ofisini kwangu kutaka kibali cha kukata mti kwa ajili ya ujenzi.

“Nilipojiridhisha, nilimpa kibali, baada kuona ameruhusiwa kujenga nyumba na mwenyekiti wa kijiji,” alisema afisa mtendaji huyo.

 

Alisema wakati mwananchi huyo akiendelea kuukata mti huo, habari zilimfikia afisa tawala wa wilaya (jina halikutajwa) ambaye alifika na kuzuia mti huo kukatwa kwa sababu unatumika kwa shughuli za kimila.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa, baada ya afisa huyo kuondoka, mkataji aliendelea kuukata mti huo hadi ukaanguka na hapo ndipo kasheshe lilipoanzia.

 

“Baadaye nilimuita chifu Mazengo akasema mbali na mti kukatwa, kwenye mti huo pia kulikuwa na nyuki wa kimizimu ambao wameondoka na kuniambia nao anataka warudishwe haraka.

“Kwa kweli nilimuambia siwezi kuwarudisha nyuki hao kwa sababu sijui wamekwenda wapi na nikamwambia twende kwenye vyombo vya sheria wakatuamulie,” alisema Pesa.

 

Aliongeza kuwa, tangu aanze kazi eneo hilo, hajawahi kuambiwa kuwa mti huo unatumika kwa mambo ya kimila na mwenye jukumu la kumuambia alikuwa yeye chifu, lakini hakufanya hivyo.

Pamoja na mambo mengine, jina la aliyekuwa waziri mkuu mstaafu wa Awamu ya Pili, John Malecela, nalo lilitajwa katika sakata hilo.

 

“Chifu Henry Mazengo amesimikwa kuwa Chifu wa pili Septemba 07, 2019 kushika nafasi iliyokuwa wazi tangu mwaka 1967 baada ya Chifu wa kwanza wa kabila la Wagogo Chaula Mazengo kufariki dunia.

“Kwenye sherehe hiyo, waziri mkuu mstaafu (Malecela) alihudhulia, kwa hiyo hili jambo siyo dogo lina umuhimu na heshima yake kwenye jamii yetu,” alisema mzee mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

 

Kwa upande wa sheria za nchi, mambo ya mila na desturi hayakatazwi isipokuwa zile ambazo zinatweza utu na kwamba kila mwananchi anao uhuru katika suala la Imani.

Stori: Mwandishi Wetu, Dodoma

Leave a Comment