×

Utata Mpya Watoto wa Diamond!

KWENYE familia ya mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ hakukauki mambo ambapo mjadala mkubwa kwa sasa ni utata mzito aliouibua yeye mwenyewe juu ya uraia wa wanaye watatu.

Watoto wa Diamond au Mondi wanaoibua mjadala mpya juu ya uraia wao ni Latiffah ‘Tiffah Dangote’ (5) na Nillan Nasibu ‘Prince Nillan’ (4) aliozaa na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Naseeb Junior (1) aliyezaa na Tanasha Donna.

Ambaye hana utata juu ya uraia wake ni Abdul Nasibu ‘Dyllan’ (4) ambaye amezaa na Hamisa Mobeto na wote ni Watanzania.

MONDI AIBUA UTATA MPYA

Mondi ambaye ni C.E.O wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), ameibua utata huo baada ya kuposti video kwenye ukurasa wake wa Instagram, akiwa ‘ana-promote’ Wimbo wa Amaboko alioshirikishwa na msanii wake, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’.

Mondi alitoa chalenji kwa mashabiki wake kurekodi vipande vya video za wimbo huo kutoka nchi mbalimbali, jambo ambalo mashabiki hao walilifanya.

Baada ya wito huo, aliposti video ya watoto maarufu ambao ni madansa wa nchini Uganda waitwao Getto Kids na kuandika;

“Uganda, unajua baba yangu anatokea huko na watoto wangu pia wanatokea huko…”

Maelezo hayo ya Mondi, yaliwashangaza mashabiki baada ya kusema baba yake, Abdul Juma ‘Baba D’ ana asili ya nchini humo.

Pia alikwenda mbali na kusema watoto wake wawili ambao ni Tiffah na Nillan, pia asili yao ni Uganda.

“Inaweza ikawa mzee Abdul asili yake ni Uganda na si Kigoma kama watu wanavyofahamu,’’ alisema shabiki mmoja.

URAIA WA TIFFAH NA NILLAN

Kupitia kauli hiyo ya Mondi, ilidhihirisha kuwa Tiffah na Nillan, chimbuko lao ni Uganda kutokana na kuwa babu yao (Baba D) ana asili ya Uganda na hata mama yao (Zari) ni raia wa nchini humo.

Inajulikana kuwa, Mondi asili yake ni mkoani Kigoma kwani hata mama yake, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’ anatokea Kigoma, hivyo ni Mtanzania.

Gazeti hili linafahamu kuwa, Tiffah na Nillan ni raia wa nchini Afrika Kusini wanakoishi na mama yao Zari katika Jiji la Durban.

Tiffah yeye alizaliwa nchini Tanzania, lakini Zari alimbadilishia uraia na kuwa raia wa Afrika Kusini. Nillan yeye ni mzaliwa wa nchini humo.

UFAFANUZI

Katika mahojiano ya gazeti hili na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, Mratibu Mwandamizi, Ally Mtanda, mwaka jana juu ya uraia wa Tiffah na Nillan, alikuwa na haya ya kusema;

“Huyo Zari kama anasema watoto hao wote ni raia wa Afrika Kusini, hakosei, yuko sahihi kwa kuwa yeye anaishi nchini humo, hivyo watoto wake wana uraia wa kurithi kutoka kwake.

“Lakini hata hivyo, kwa kuwa watoto hao baba yao ni Mtanzania, pia wana uraia wa Tanzania ambao wameurithi kutoka kwa baba yao, hivyo wana uraia wa nchi mbili na wanaruhusiwa kuwa na pasipoti ya Tanzania na Afrika Kusini kwa wakati mmoja.

“Watoto watatakiwa kuukana uraia wa nchi moja na kubaki na uraia wa nchi moja baada ya kutimiza umri wa miaka 18 ambapo watakuwa na uamuzi wa kuchagua uraia wa baba au mama yao.”

URAIA WA UGANDA

Kwa hiyo, utata mpya wa Tiffah na Nillan ni juu ya kuwa raia wa Uganda kama alivyosema Mondi, kwani kama watataka kuwa raia wa nchi hiyo, itabidi waukane ule wa Afrika Kusini watakapofikisha umri wa miaka 18.

Hata hivyo, kama watataka kuwa na uraia pacha; yaani wa nchi mbili, hilo halitawezekana kwani Katiba ya Uganda hairuhusu aina hiyo ya uraia hivyo kuzidi kuongeza utata.

URAIA WA NASEEB JUNIOR

Naseeb yeye amezaliwa nchini Tanzania, lakini Tanasha ambaye ni raia wa nchini Kenya, alisepa naye baada ya kushindwana na Mondi mapema mwaka huu.

Kuna madai yaliibuka kuwa, Tanasha alikuwa anafanya mpango wa kumtafutia Naseeb cheti cha kuzaliwa cha nchini Kenya.

Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania; “Mtu yeyote anayezaliwa kwenye ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huyo ni raia kamili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama wakati wa kuzaliwa wazazi wote au mmoja ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

URAIA WA KENYA

Kama ilivyo Afrika Kusini, Kenya inaruhusu mtu kuwa na uraia wa nchi mbili, tofauti na Tanzania, hivyo inawezekana Naseeb akawa na uraia wa Tanzania na Kenya kwa wakati mmoja.

TUJIKUMBUSHE

Hii si mara ya kwanza kwa wasanii kusikika wakisema kuwa, wazazi wao si Watanzania kwani hata mwanamuziki Rajab Abdul ‘Harmonize’ aliwahi kusema kuwa mama yake ana asili ya nchini Nigeria.

 

STORI | Happyness Masunga, Risasi

Leave a Comment